DODOMA: MBWA wa ajabu watatu wametikisa jijini Dodoma baada ya kumshambulia mtoto mmoja anayefahamika kwa jina la Akisa Wilson Moyo, mwenye umri wa miaka saba, mkazi wa Kata ya Ipagara, Mtaa wa Ilazo mkoani hapa hivi karibuni. Mtoto huyo, kutokana na shambulio hilo, amepata majeraha makubwa sehemu mbalimbali za mwili wake. Hilo ni tukio la tatu kufanywa na mbwa hao ambao hajulikani mmiliki wake.
Akizungumza na gazeti hili, shuhuda mmoja ambaye pia ni baba mzazi wa mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina la Kalsoni Mzava alisema kuwa, mtoto wake huyo alishambuliwa na mbwa hao majira ya jioni, wakati akielekea kwenye mkutano wa Injili uliokuwa unaendelea takriban mita mia sita kutoka nyumbani kwao.
Aliongeza kuwa, baada ya kutokea kwa tukio hilo alikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi cha Kati ‘Sentro’ mkoani hapo na alipewa Fomu ya Matibabu (PF-3) kisha mtoto huyo alimkimbiza Hospitali ya Mkoa wa Dodoma (General) ambako alilazwa wodi namba tano. Alisema kuwa, Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ambaye hakulifahamu jina alitoa watu wa manispaa na kitengo cha mifugo kuwafuatilia mbwa hao.
”Ajabu ni kwamba hili tukio siyo la kwanza kutokea kwenye mtaa wetu, hii ni mara ya tano sasa matukio haya yanafululiza. Hawa mbwa wa ajabu wamekuwa tishio kwa kweli kwani wanamkamata mtu na wanamvutia porini mithili ya simba na kumtafuna.
“Sisi wakazi wa mtaa huu tunasema, ikiwa hatutapata msaada wa kuwaua mbwa hawa, watatuua raia wa hapa,” alilalamika Mzava. Aliongeza: “Tunaliomba Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma na Mkuu wa Mkoa na kamati yake ya ulinzi na usalama itutatulie tatizo hili kwa kuwaua mbwa hawa ambao wanatikisa, haraka iwezekanavyo kwani wanazidi kuumiza watu hapa mtaani kwetu.
“Naongea kwa uchungu kwani mtoto wangu tumemuokoa wakati akiwa ameshavutiwa porini, tusingemuwahi, angeuawa na mbwa hawa. Natoa tahadhari kwa wazazi mtaani kwetu kuwachunga watoto wao kutokana na hatari ya mbwa hawa.” Aidha mmoja wa wakazi wa Dodoma aliyejitambulisha kwa jina la Sudi alisema kuwa, mbwa hao wamekuwa wakihusishwa na mambo ya kishirikina kutokana na namna wanavyoibuka na kushambulia watoto.
“Hawa mbwa siyo wa kawaida, ndiyo maana wengine tunaona kuna mambo ya kishirikina katika matukio kama haya,” alisema Sudi. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, SACP Gilles Muroto hakupatikana kwa njia ya simu alipotafutwa na gazeti hili wakati tunakaribia kwenda mitamboni.
STORI: JACQLINE OISSO, RISASI JUMAMOSI