Mke wa Sugu Alivyobuni Keki ya Picha ya Gereza Kwenye Birthiday ya Mumewe

Mke wa Sugu Alivyobuni Keki ya Picha ya Gereza Kwenye Birthiday ya Mumewe
Utamaduni wa sherehe ya kuzaliwa ulianza bara la Ulaya miaka mingi iliyopita. Ilikuwa ikiogopewa kwamba mashetani walivutiwa zaidi kwa watu katika siku zao za kuzaliwa, ili kuwalinda na madhara.

Ndugu na marafiki hujumuika kwa mwenye kusherehekea siku ya kuzaliwa wakiwa na maneno yenye faraja na matumaini na pia maombi.

Pia, sherehe hizo hupambwa kwa zawadi zenye lengo la kuleta furaha, uchangamfu na zaidi ya hapo zimelenga kuwafukuza mashetani hao. Sherehe za kuzaliwa zilienea hadi katika nchi za Afrika na siku ya Mei Mosi, mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alikuwa akisherehekea siku yake.

Siku hiyo alikuwa akitimiza miaka 46. Hata hivyo, aliisherehekea siku hiyo akiwa kifungoni katika gereza la Ruanda jijini Mbeya anakotumikia kifungo cha miezi mitano.

Sugu alihukumiwa kifungo hicho pamoja na katibu wa Chadema wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga Februari 26 baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mbeya kuwakuta na hatia ya kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli. Waslidaiwa kufanya kosa hilo Desemba 30 mwaka jana.

INAENDELEA UK 22

INATOKA UK 21

Sherehe ya Sugu nayo haikukosa zawadi. Kwanza kuliandaliwa keki aliyopelekewa gerezani kama zawadi maalumu kwake, na akasherehekea siku yake muhimu kwa kula chakula pamoja na watoto yatima wa kituo cha Nuru kilichopo Uyole pamoja na kutoa msaada wa maziwa ya watoto na nguo.

Familia ya Sugu, ikiongozwa na mke wake, Happines Msonga, ilimfanyia jambo hilo kwa kumshtukiza. Pia waliambatana na wafanyakazi wa Hotel ya Desderia inayomilikiwa na Sugu pamoja na wafuasi wa Chadema

Keki ilichorwa pingu, mnyororo na taswira ya chumba cha gereza na picha yake ikimuonesha yupo ndani ya chumba hicho na mtu anamuona kupitia nondo za chumba.

Pia ilikuwa na ua aina ya waridi kuashiria mahaba ya mke kwa mume.

Baadaye, familia ya Sugu ilisherekea siku hiyo kwa kwenda kula chakula pamoja na watoto wa kituo hicho cha Nuru kama walivyoagizwa na Sugu kwa uongozi wa hoteli hiyo.

Kwanini watoto yatima?

Pengine swali linaweza kuwa kwa nini kituo cha Nuru na kwa nini iwe kituo cha watoto yatima.

Akizungumza na Mwananchi, Happines alisema mumewe ndiye aliyeagiza kwamba siku ya kuzaliwa kwake iadhimishwe pamoja na watoto yatima kwa kula nao chakula cha pamoja.

Alisema aliamua kufanya hivyo ili kuendelea kuwa karibu na wananchi wake katika shughuli za kijamii hata kama yupo gerezani kwa kuwa anao ajibu wa kuwatumikia wananchi wake.

“Sote tunajua yupo gerezani lakini amesema anawapenda sana watoto na wananchi wa jimbo lake kwa ujumla na kiroho yupo nao daima,” alisema Happiness.

“Alisema kwa kuwa siku yake ya kuzaliwa ni Mei Mosi, ni vyema tukashiriki sherehe hiyo na watoto yatima.”

Anasema kufanya hivyo ni mwendelezo wa Sugu kuwatumikia watoto yatima kama anavyofanya kwa kutumia mfuko wake wa kuwasomesha watoto yatima katika shule za sekondari zilizopo ndani ya jimbo la Mbeya Mjini.

“Sote tunajua kuwa Sugu ana mfuko ule wa kusomesha watoto kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne. Hivyo uongozi wa Hotel Desderia ambayo anaimiiliki imeanzisha mpango maalumu wa kuwatembelea na kujumuika na watoto wanaolelewa kwenye vituo vyote vilivyopo jijini hapa kila mwisho wa mwezi kwa kuwapelekea chakula na misaada mingine,” alisema.

Keki ilivyopambwa

Happiness anasema alibuni umbo la keki hiyo kwa lengo la kuonyesha mume wake anasherekea siku yake ya kuzaliwa akiwa gerezani, hivyo ilikuwa ni ishara kwamba bado yupo ndani lakini familia yake na wananchi wa jimbo lake wanamkumbuka na kuendelea kumpenda.

“Wazo la kutengeneza keki ikiwa na muonekano ule lilikuwa langu mwenyewe,” alisema.

“Lakini kubwa zaidi ile ilikuwa ni Surprise kutoka kwangu maana sikumuambia kuwa nitamuandalia chochote. Hivyo siku ile nilipompelekea na kufungua boksi, hakuamini kabisa na hasa alipoona pingu, mnyororo na picha yake inayomuonyesha yupo kwenye chumba cha gereza chenye nondo.”

“Hata siku akitoka gerezani, nitamuandalia keki ambayo itakuwa imechorwa ikionyesha zile pingu zimekatika na milango ya gereza imefunguliwa na hii yote ni kuonyesha kwamba sasa yupo huru na amerejea nyumbani kuungana na familia yake pamoja na wananchi wake wa jimbo la Mbeya Mjini.”

Mkurugenzi mtendaji wa kituo cha Nuru, Jarson Fihavango alimshukuru Sugu na uongozi mzima wa hoteli yake kwa kuwapelekea chakula na misaada mingine watoto wanaolelewa kituoni hapo.

“Tunajua mbunge wetu alipatwa na matatizo, lakini pamoja na kwamba yupo mahali ambapo si nzuri sana ila bado anawakumba wananchi wake. Na sisi tunashukuru sana kwa hiki alichotufanyia,” alisema.

“Tunasema aendelee na moyo huohuo na sisi tunamuombea. Hiki alichokifanya kina Baraka kubwa mbele za mwenyezi Mungu, tunajua namna anavyoweza kumlipa’.

Fihavango anasema sio kazi rahisi kwa mtu ambaye yupo kwenye matatizo, lakini akawa na roho ya kuwakumbuka watu wake wa walio nje na kuwatumikia kama kawaida.

Katibu wa mbunge

Tangu alipofungwa Sugu amekuwa akiwatumikia wananchi wake wa Mbeya Mjini kupitia kwa wawakilishi wake akiwamo katibu wake, Gideon Siame.

Siame anasema pamoja na bosi kuwa gerezani amekuwa akitekeleza majukumu kwa wananchi wa jimbo hilo kama kawaida huku akiwa anapelekewa taarifa zote na kutoa maelekezo pale inapobidi.

“Kinachoendelea ofisini ni zile shughuli tu za kawaida ambazo hata yeye (Sugu) akiwa Dodoma au nje ya jimbo, huwa tunakuwa tunaendelea nazo. Kuna mambo ambayo huwa yanahitaji tumshirikishe kwa ajili ya mawazo yake au maelekezo huwa tunafanya hivyo,” alisema katibu huyo.

“Na hivi sasa yupo gerezani pale tunapopata nafasi ya kumuona huwa tunamueleza kinachofanyika na yeye anatupa mawazo na maelekezo yake.”

Anasema kila wanapopata muda wa kumuona gerezani, Sugu amekuwa akiwasisitiza kuendeleza harakati za kulikomboa taifa na akiwataka wasiteteleke kwa kuona viongozi wa kisiasa wanafunguliwa kesi na kufungwa kama yeye, bali iwe chachu ya kupigania ukombozi.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad