Kiongozi wa chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change (MDC) nchini Zimbabwe, Nelson Chamisa amesema kuwa atawafukuza wawekezaji wote kutoka China nchini humo endapo atachaguliwa kuwa Rais kwenye uchaguzi mkuu mwezi Julai mwaka huu.
Chamisa amesema kuwa Wachina wamekuwa wakitorosha rasilimali za nchi hiyo na uwekezaji wao umegubikwa na rushwa hivyo haoni sababu ya kuwaruhusu kufanya kazi nchini humo.
“Wawekezaji kutoka china ni moja ya watu wanaolifilisi taifa letu, wanachukua rasilimali zetu kwa kisingizio cha uwekezaji na wamesaini mikataba ya hovyo na serikali ya Zanu-PF sioni umuhimu wao ni bora tukaacha hizo rasilimali zikatumiwa baadae nawaahidi mkinichagua kuwa rais nitawafukuza wawekezaji wote Wachina na wengine ambao wataonekana na mikataba kama hiyo nitawatimua, tumechoka kunyonywa,“amesema Chamisa juzi Mei 01, 2018 mjini Harare kwenye maadhimisho ya siku yawafanyakazi duniani.
Zimbabwe inatajwa kuwa ni nchi ya nne barani Afrika kuwa na wawekezaji wengi kutoka China, na hoja hiyo inaungwa mkono na wabunge wengi hata wale wa chama tawala cha ZANU-PF.
Uchaguzi huo mkuu utakuwa uchaguzi wa kwanza na wa kihistoia nchini humo tangu utawala wa Robert Mugabe kuangushwa mwezi Januari mwaka huu.
Chamisa alitangazwa kuwa kiongozi wa chama cha MDC mwezi Februari akimrithi aliyekuwa kiongozi wa chama hicho, Morgan Tsvangirai baada kufariki dunia.
Mpinzani mkubwa wa Chamisa ni Rais wa sasa wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa maarufu kwa jina la ‘Ngwena’ yaani MAMBA .