Mwakyembe Noma, Afukua Utajiri wa Marehemu Kanumba

Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison George Mwakyembe

SIFA anazomwagiwa Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison George Mwakyembe mitaani, zinatosha kusema kuwa waziri huyo ni noma katika uchapakazi wake.

Dawati la Ijumaa ambalo kila siku halipoi kusaka habari ziliokwenda shule limebaini kuwa Dk Mwakyembe amekuwa kiongozi anayetajwa na wananchi wengi hasa wasanii kuwa anamudu kuingoza wizara iliyo chini yake.

Ukaribu wake na wasanii wa muziki wa ladha tofauti, ufuatiliaji wa masuala ya michezo ukiwemo mpira wa miguu, ngumi, riadha na usimamiaji wa haki za wasanii kwa jumla ni miongoni mwa mambo yanayompandisha chati waziri huyo.

 HABARI ILIYOBAMBA

Hivi karibuni, Dk Mwakyembe, akiwa bungeni jijini Dodoma, aliliamsha dude kwa kuahidi kufuatilia kwa kina mikataba yote isiyokuwa na tija kwa wasanii ambayo hatimaye huyaacha maisha yao kwenye ufukara.

Ahadi ya ufuatiliaji huo wa mikataba feki ilichochewa na waziri huyo kuguswa na hali ya ugonjwa na changamoto za kimatibabu zinazomkabili mwigizaji mkongwe nchini, Amri Athuman ‘Mzee Mjuto’ ambaye kwa sasa yuko nchini India kwa matibabu.



“Leo hii Mzee Majuto anaumwa, anaomba pesa, ninachanga pesa kutoka mfukoni kwangu, lakini leo hii nusu ya mabango ya biashara, matangazo ya biashara kwenye TV ni Majuto, ninaomba sasa nitumie nafasi hii kusema nimeunda kamati ya wanasheria, tunaanza na kesi ya Majuto. Mashirika yote, kampuni zote zilizoingia mkataba na Majuto, tutapitia hiyo mikataba, kama ameonewa lazima ilipwe familia yake…tumechoka.



“Tukishamaliza na Majuto tunarudi na kwa Kanumba (marehemu Steven Kanumba) na msanii yeyote ambaye anaona ameingia mkataba wa kipumbavu, aje tuone. Mheshimiwa mwenyekiti inaudhi, lakini ndiyo hivyo.

“Leo hii Mzee Majuto yuko hospitalini, amekosa shilingi laki tano, nimtumie mimi wakati waziri pesa yenyewe ndiyo hiyo mnaelewa, eeh…maisha siyo…”

 IJUMAA NA DK MWAKYEMBE KATIKA MAZUNGUMZO

Baada ya tamko hilo la waziri huyo anayetaka kuuvunja mfupa uliowashinda mawaziri wenzake wengi wa kuwafanya wasanii wa Kibongo nao kula bata kupitia kazi zao za sanaa, gazeti hili lilizungumza katika mahojiano maalum na kutaka kujua amefikia wapi katika kushughulikia mikataba au naye amepoa?



Fasta bila kuchelewa, waziri huyo alipokea simu yake ya mkononi iliyopigwa na Mwandishi Wetu saa 7: 24 mchana wa Mei 9, mwaka huu na hapo ndipo alipofungua kabrasha la taarifa kamili juu ya kauli yake hiyo.

MSIKIE DK MWAKYEMBE

“Zoezi limeshaanza, kwa sababu suala la mikataba linahitaji umakini, weledi na kusimamia haki, nimeshaunda timu ya wanasheria watano ambao wanapitia hiyo mikataba.

“Lakini kwa sababu suala lenyewe ninahitaji liende haraka, ninakusudia kuongeza wanasheria wengine wanne ili wafikie tisa, lakini kwa sasa hao watano wameshaanza kuchambua baadhi ya mikataba inayolalamikiwa na wasanii wetu.

“Ninachoweza kukuambia ndugu yangu ni kwamba, katika hiyo mikataba tuliyopokea, tayari kuna mingine imeshachambuliwa na atumefikia hadi hatua za kuwakutanisha walalamikaji na wanaolalamikiwa, kwa hiyo zoezi linakwenda vizuri,” alisema Dk Mwakyembe wakati akijibu baadhi ya maswali aliyoulizwa na Mwandishi Wetu.

 ATOA WITO KWA WASANII

Aidha, Waziri Mwakyembe, mbali na kueleza kuwa atajitokeza hadharani hivi karibuni kuwaambia wananchi kile atakachovuna katika kazi yake hiyo aliyoianza amewataka wadau wa sanaa wenye mikataba yenye shaka wajitokeze ili matatizo yao yatafutiwe ufumbuzi.

Wito huo ulitolewa na waziri huyo baada ya gazeti hili kutaka kujua wizara yake iko ‘siriaz’ na mikataba ya Kanumba na Majuto peke yake au na wasanii wengine wanaweza kujiunga katika msafara huo aliouanzisha wa kuuangamizi unyonyaji.

MITAANI KWA WASANII KUKOJE?

Baada ya waziri kuliamsha dude, gazeti hili lilipita katika ulimwengu wa sanaa na kuwaangalia wasanii wenyewe wameipokeaje hatua hiyo ya waziri ambapo ilibainika kuwepo kwa vicheko na nderemo.

Mama mzazi wa msanii maarufu aliyega dunia miaka sita iliyopita, Steven Kanumba aitwaye Flora Mtegoa ni miongoni mwa watu waliofurahia hatua hiyo ya waziri.



“Mwanangu amefariki dunia, ameacha mikataba mingi kwenye makampuni, lakini hakuna nilichopata, kuna siku nilikwenda kwenye kampuni (anaitaja lakini tunahifadhi jina) kuulizia, nilipofika waliniambia Kanumba alishakufa na mikataba yake ilishakufa pia.

“Yaani sijui nikuambie nini, nimefurahi kusikia waziri anatafuta haki za mwanangu, najua kwa sasa yuko bungeni, akitoka huko nitakwenda kumuona,” alisema mama Kanumba.



Mbali na mama Kanumba, mwingine ambaye Ijumaa lilinasa habari za kulalamikia mkataba feki ni Wastara Juma ambaye mara kadhaa amekuwa akijitokeza na kudai kudhulumiwa kiasi cha shilingi milioni 80 na Kampuni ya KZG ya China.

Wastara anadai kuwa, KZG ilimpa mkataba wa kuwa balozi wa bidhaa za simu ya mkononi kwa makubaliano ya kiasi hicho cha fedha, lakini baadaye kampuni hiyo ilitimka nchini na kurejea China huku ikimwacha Wastara akilia.

 WANASHERIA WAFUKUA UTAJIRI WA KANUMBA, MAJUTO

Habari za chini ya kapeti zilizonaswa na gazeti hili zilidai kuwa, timu hiyo ya wanasheria walioteuliwa na Waziri Mwakyembe wameshaanza kufukua mikataba yote ya Kanumba na Majuto na endapo hali ikiwa upande wa wasanii hao, huenda utajiri ukawatembelea licha ya Kanumba kutokuwepo duniani na Majuto kuwa hospitalini huko India.

Kwa miaka kadhaa, kumekuwepo na kesi mbalimbali za wasanii wa Bongo kudhulumiwa haki zao, jambo ambalo kwa sasa linaonekana kuanza kupatiwa tiba na huenda likawatajirisha wasanii wengi.

 TUPEKUE KIDOGO HABARI HII

Pamoja na nia njema ya waziri ya kuwasaidia wasanii kupata haki katika mikataba feki, Timu ya Ijumaa inaungana na Waziri Mwakyembe na kumshauri kuwa jambo hilo linahitaji umakini mkubwa kulishughulikia kutokana na aina, maisha na uelewa wa wasanii wengi hapa nchini.

Kutokana na uzoefu na kuishi karibu na wasanii wa Bongo, gazeti hili limebaini kuwa maisha ya ‘njaanjaa za kujiendekeza’ yamekuwa yakisababisha baadhi ya wasanii kuingia mikataba feki ili kujipatia fedha hata kiduchu za kufanyia matanuzi mjini angalau kwa siku moja.

Kwa msingi huo, gazeti hili linawataka wasanii wa Bongo kutambua hadhi yao, kujielimisha kuhusu mikataba, kuacha tabia za kuingia mikataba kwa lengo la kukidhi shida ya siku moja.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad