Matukio ya watu kujichukulia sheria mikononi yamesababisha vifo vya watu wawili mkoani Mtwara, likiwamo la mke kumuua mumewe katika ugomvi wa kudai chakula.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, kamanda wa Polisi mkoani hapa, Lucas Mkondya alisema Mei 22, saa 1:30 usiku katika Kata ya Namuyonga wilayani Newala, polisi iliwakamata watu wawili wakituhumiwa kumuua Ahmad Salum kwa kumchoma kisu kifuani.
Alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kabla ya mauaji ulitokea ugomvi kati ya Salum na mkewe ambaye ni miongoni mwa waliokamatwa.
Mkondya alisema mwanamke huyo alikataa kupika chakula kingine baada ya mumewe kumweleza hakushiba, hivyo uliibuka ugomvi.
Alisema mtuhumiwa mwingine ambaye ni jirani alikwenda nyumbani kwa wanandoa hao na anatuhumiwa kushirikiana na mke wa Salum katika mauaji hayo. “Nitoe rai kwa wananchi ugomvi hauna tija wakae wajaribu kusuluhishana lakini si kugombana kwa kitu kidogo kama chakula mpaka inafikia mtu kupoteza maisha, lakini pia wanaweza kuwatumia majirani na viongozi wa kiserikali katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kutatua matatizo yaliyopo katika familia,” alisema.
Katika tukio jingine, Mkondya alisema mkazi wa Nanyamba wilayani Mtwara, Athuman Kidakwa aliuawa na watu wasiofahamika kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali na mwili kuchomwa moto.
Kamanda alisema Athuman alikuwa mfungwa aliyetoka jela kwa msamaha wa Serikali.
Alisema mtu huyo alituhumiwa kuiba simu na kwa kuwa alishafungwa wananchi walimshambulia na kumuua.
Kamanda alisema wanaendelea kuwatafuta watu waliohusika na mauaji hayo kwa kujichukulia sheria mkononi.
“Huyu alichomwa na kitu chenye ncha kali na wananchi. Inasemekana alikuwa mwizi na hivi karibuni alitoka jela kwa msamaha wa Serikali, lakini baada ya kutoka akaenda kukwapua simu ya mtu basi kundi la watu kwa sababu wanamfahamu walimshambulia,” alisema.
Aliwaonya wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kutaka watu wanapotenda makosa watoe taarifa polisi.