Mwanaume mmoja ameshitaki kanisa moja nchini Uganda akipinga kanuni za utaratibu wa kufunga ndoa akieleza kuwa zinakwenda kinyume na katiba.
Michael Aboneka amepeleka kesi hiyo katika mahakama ya katiba mjini Kampala kulishtaki kanisa la Watoto Church wakati waumini wengine wa kanisa hilo wakiunga mkono taratibu za kanisa lao.
Michael Aboneka amesema kuwa Watoto Church, linawanyima vijana wengi haki yao ya kikatiba ya kufunga ndoa na wapenzi wao baada ya kutimiza umri wa miaka 18 kama katiba ya Uganda inavyosema.
Ameeleza kuwa baada ya kuzisoma kanuni hizo za kufunga ndoa, ameona kuwa zinakwenda kinyume na katiba.
'Kwanza wanasema nilazima upate barua kutoka kwa wazazi wa bibi harusi ambayo wanaita Baraka. Kwangu inakwenda na kinyume cha katiba kifungu 31 ya ndoa ya pili ni kukabidhi barua ya Dakitari ya majibu ya kupima virusi vya ukimwi kwa kanisa'.
'Nimekwenda hospitalini kupimwa na mchumba wangu tumepata majibu tunafahamu majibu ya kila mmoja wetu. Kwa hiyo mimi na mchumba wangu kukabidhi vipimo vya ukimwi kwa kanisa inavunja haki ya uhuru wa siri zetu, nimekuta ni kinyume na katiba'. amesema Aboneka.