Mwigulu Aagiza BodaBoda Zilizokamatwa na Polisi Ziachiwe Mara Moja

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ameagiza pikipiki zote (bodaboda) ambazo zinashikiliwa na polisi kwa makosa madogo ziachiwe mara moja na wahusika wapewe nafasi ya kwenda kutafuta faini wakiwa na vyombo vyao.

“Naagiza kuanzia leo na nitapita kuangalia maeneo mbalimbali pikipiki ambazo hazihitajiki kwenda mahakamani kwa ajili ya kutolea ushahidi nataka ziachiwe mara moja ili kuwapatia wenye mali,” amesema Dk Mwigulu.

Awali, Spika Job Ndugai alimtaka Waziri huyo kufanya sensa ya kutosha na kujionea namna ambavyo vijana wengi wamekuwa wakipoteza mali zao kwa kukamatwa na polisi katika maeneo mbalimbali katika makosa madogo tu.

Ndugai amesema Serikali inapoteza fedha nyingi kupitia kwa waendesha bodaboda na kuwafanya wengi kuwa maskini huku akitolea mfano wa kituo kikuu cha polisi cha mkoa wa Dodoma ambapo amesema kuna pikipiki zaidi ya 300 zinashikiliwa lakini hazina makosa makubwa.

Awali, Mbunge wa Mpwapwa (CCM) George Lubeleje aliomba mwongozo wa Spika kuhusu suala la faini kwa madereva wa bodaboda na kumtaka kutoa maagizo kwa jeshi la polisi ili kupunguza kamatakamata hiyo.

Lubeleje amesema polisi wamekosa huruma kwa vijana wa Tanzania ambao wamekuwa wakilia kwa kushilikiliwa vyombo vyao bila makosa makubwa na hivyo akaomba waruhusiwe kwenda kutumia pikipiki hizo kutafuta faini wanazodaiwa na polisi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad