WAKATI ikitajwa kuwa huenda beki kisiki wa Yanga, Kelvin Yondani akatimka ndani ya kikosi hicho, Katibu wa Baraza la Wazee wa klabu hiyo, Ibrahim Akilimali, amefunguka kuwa ni bora waondoke wachezaji wote lakini si Yondani, sababu atamwaga machozi.
Yondani, mkataba wake unamalizika ndani ya klabu hiyo na amekuwa akihusishwa kuwa huenda akatua katika Klabu ya Azam ambapo inadaiwa kuwa anahitajika kwenda kufanya kazi na kocha mpya ya timu hiyo, Mholanzi, Hans van Der Pluijm.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mzee huyo alisema kuwa anaumia sana anavyozisikia taarifa hizo na anamuomba beki huyo kubaki hapo.
Akilimali alienda mbali zaidi na kudai beki huyo amekuwa na msaada mkubwa ndani ya klabu hiyo.
“Kama hizo taarifa ni za kweli Yondani ataondoka basi binafsi nitalia sana, sababu ni moja, kati ya wachezaji ambao walikuwa wanacheza kwa nguvu kubwa, alijituma bila kuangalia klabu ipo kwenye hali gani basi ni Yondani.
“Waondoke wachezaji wote lakini siyo yeye, itaniuma sana, siyo siri kwa jinsi ambavyo namfahamu mjukuu wangu, nimekuwa nikiongea naye mambo mengi kutokana na kuipenda timu na kujituma,” alisema Akilimali.