SERIKLI kupitia kwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile imekataza Mamlaka ya Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), kuruhusu watu au taasisi zisizo na mamlaka kisheria kuwaamuru kupima sampuli za vinasaba (DNA).
Dkt. Ndugulile aliyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa Bodi Tendaji ya GCLA yenye wajumbe saba kutoka Wizara yake, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Katiba na Sheria na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) huku akiziitaka mamlaka hiyo kutoa elimu kwa jamii kuhusu majukumu ya mamlaka hiyo, ili kuepuka watu au taasisi kutoa maagizo juu kwa mamlaka hiyo kinyume cha sheria na taratibu.
“Tusiamini kila mtu anajua utaratibu. Tunaweza sasa kuja kuvumbua mambo ambayo hayapo. Si kila mtu anaweza kuamrisha Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuchukua vipimo vya DNA, si hivyo kuna taratibu zake,” alisema.
Dkt. Ndugulile alisema lazima wananchi waelezwe taratibu zikoje, nani anawajibika kwenda kupeleka sampuli na nani ana wajibu huo kwa sababu majukumu yake ni ya kisheria huku akieleza katika siku za karibuni suala la kupima vinasaba limezungumziwa sana hali ambayo imezua mkanganyiko kwa jamii, hivyo kuitaka mamlaka hiyo kutimiza wajibu wa kutoa elimu.
Licha ya kutokumtaja mtu aliyetoa amri ya watu kupimwa DNA, hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliwaita watu waliodaiwa kutelekeza watoto kujitokeza ambapo baadhi yao walijitokeza, lakini 90 kati ya wanaume hao, waliwakana watoto waliodaiwa kuwa wamewatelekeza na kutaka waende wakapimwe DNA katika maabara ya Mkemia Mkuu ili kumaliza utata huo.
Katika hatua nyingine, Dk. Ndugulile aliitaka taasisi hiyo kuwa na mkaguzi wa kimataifa wa ubora wa sampuli wanazopima, ili zikubalike kitaifa na kimataifa.
“Lazima muwe na mkaguzi wa kimataifa wa kuthibitisha kile mlichopima kwa sababu taasisi hii ina majukumu ya kisheria ya kuamua ukweli kuhusu sampuli iliyopimwa. Mkisema huu ni unga wa mahindi ilhali tunaona ni dawa za kulevya hatuwezi kupinga,” alisema.
Pia aliitaka mamlaka hiyo kutoa majibu kwa wakati, ili kupunguza kesi zilizopo mahakamani zinazosubiri majibu ya maabara hayo.Alisema, ili kutekeleza agizo hilo, amewataka kuandaa mikataba inayoonyesha kazi itakamilika kwa muda gani pindi wanapopokea sampuli.
“Utakumbuka kuna wakati kesi zilirundikana katika mahakama zetu hivyo mnatakiwa kufanya kazi kwa haraka na kwa wakati na muwe na mikataba inayoonyesha kazi itakamilika kwa muda gani,” alisema.
Aidha, aliwataka kuwatambua wale wote wanaojihusisha shughuli za kemikali nchini wakiwamo, wauzaji, wanunuzi na wanaozitumia kwa ajili ya kupunguza matukio ya uhalifu nchini. Kadhalika aliwataka kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi na Mazingira (NEMC) kuthibiti majitaka katika viwanda, ili kuepusha madhara kwa watu.
“Sijawasikia mkipima maji taka yanayotiririka viwandani mmekaa kimya kama si wajibu wenu, hakikisheni mnashirikiana nao na kuchukua sampuli nyie wenyewe mpime na mtoe majibu,” alisema.
Naye Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Fidelice Mafumiko, alisema GCLA inakabiliwa na uhaba wa watumishi takribani 200 na pia uchakavu wa mitambo ya kimaabara. Dk. Mafumuko pia alisema fedha za bajeti ya serikali ya mwaka 2017/18 zilizotengwa kwa ajili ya kununua mitambo na vifaa vya maabara hiyo hazijatoka hadi sasa hali ambayo inawafanya kushindwa kutekeleza majukumu yako kikamilifu.
Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Prof. Ester Jason, aliahidi kuisumbua wizara hiyo kuhusu kutekeleza majukumu ya mamlaka ikiwa ni pamoja na kutoa fedha mapema iwezekanayo.