Nape Awapa Somo Mawaziri wa JPM

Nape awapa somo Mawaziri wa JPM
Mbunge wa Mtama (CCM) Nape Nnauye, amewataka Mawaziri katika serikali ya awamu ya tano kuwa na tabia ya kusikiliza ushauri na kukubali kukosolewa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.


Nape amesema hayo leo Mei 25, 2018 Bungeni Jijini Dodoma, wakati wa kuchangia hoja mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Nishati na kuwataka Mawaziri hao kuiga mfano wa Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani na Naibu wake kwani ni watu ambao wanakubali kupokea ushauri.

“Wito wangu kwa Mawaziri wengine igeni mfano wa Kalemani, ukiambiwa jambo usilolipenda, wewe ni kiongozi kubali, sikiliza, mimi naamini Kalemani atakwenda vizuri, zipo changamoto kwenye Wizara yako, lakini ninaamini ukiendelea kuwa msikivu yale ambayo yapo juu ya uwezo wako mimi najua watu watakusamehe, lakini yale ambayo yapo ndani ya uwezo wako ukisikiliza na ukayatekeleza tutakuunga mkono” amesema Nape.

Mbunge huyo aliendelea kumwaga sifa kwa Waziri Kalemani kwa kufanikiwa kuiunganisha Mikoa ya Lindi na Mtwara katika Gridi ya Taifa pamoja na kupeleka Meneja wa TANESCO katika Mkoa wa Lindi.

Kwa upande mwingine Nape ameishauri serikali kuangalia uwezekano wa kuligawa Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) ili liweze kufanya kazi kwa ufanisi kwa kutenganisha majukumu ya uzalishaji na usambazaji na kutaka serikali kuingia ubia na sekta binafsi ili umeme uzalishwe katika kiwango kikubwa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad