Sugu amesema hayo leo Mei 21, 2018 katika viwanja vya Bunge Jijini, Dodoma ikiwa ni kikao chake cha kwanza cha bunge kuhudhria tangu ameachiwa huru baada ya kuhudumu kwa siku 73 katika Gereza la Ruanda, Mbeya, ameongeza kwamba bila kujali ni nani amempa msamaha lakini anastahili kuombwa msamaha kwa hukumu aliyopewa.
“Mimi naamini sikutakiwa kuwa ndani, na unapozungumzia suala la msamaha nabaki najiuliza, napewaje msamaha na mtu ambaye amekufunga, mtu ambaye wanasema ulimfedhehesha, kitu cha msingi sio nani kanipa msamaha, mimi siamini kana nastahili kupewa msamaha bali natakiwa kuombwa msamaha kwa kufungwa kiholela na kutoka kiholela” amesema Sugu.
Mbunge huyo ameongeza kuwa wafungwa pamoja na askari katika Gereza la Ruanda walishangaa kumuona mbunge huyo katika Gereza hilo, Sugu amesema “wafungwa na askari walinipokea vizuri, kwanza walishtuka sana kuona Mbunge ameletwa kwa kesi ambayo haileweki kwahiyo nilikuwa na kazi kama kiongozi ya kuwatuliza”
February 26, 2018 Mahakama ya Hakimu mkazi Mbeya iliwatia hatiani Sugu na Emmanuel Masonga Katibu wa CHADEMA nyanda za juu kusini na kuhukumiwa kifungo cha miezi mitano jela kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli, lakini wawili hao waliachiwa huru Mei 10, 2018 kwa msamaha wa Rais Magufuli alioutangaza katika sherehe za sikukuu ya Muungano April 26, 2018.