Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema wahifadhi wamekuwa ni walafi mno wa ardhi kwa kutaka maeneo makubwa nchini.
Amesema hayo bungeni leo Jumanne Mei 22, 2018 baada ya mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2018/19.
Ndugai amesema wanapokwenda watu wa hifadhi wanakuwa na wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambao hupima ardhi baada ya kukubaliana na wananchi.
Hata hivyo, Ndugai amesema wakati wanaporudi ofisini wanaongeza eneo bila kuwataarifu wananchi na baada ya miaka 10 hupita maeneo husika na kuwaeleza kuwa mpaka upo maeneo mengine.
“Si waseme (wawambie wananchi) mimi mwenyewe ni mhifadhi tatizo sisi wahifadhi ni walafi mno wa ardhi,” amesema.
Awali, Profesa Tibaijuka akichangia amemweleza Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla kuwa yeye (Kigwangalla) ni daktari wa binadamu na kwake ni kulinda maisha ya watu, lakini kwenye masuala ya hifadhi kunamuangusha kutekeleza umuhimu huo.
“Rais wetu anawalinda wanyonge lakini majirani wa hifadhi si wanyonge. Kusema ukweli hali ilivyo si hivyo,” amesema.
Amemshauri Dk Kigwangalla kuachana na misitu ya akiba na mapori ya akiba, kwa sababu yamepitwa na wakati badala yake atangaze Hifadhi ya Taifa ambayo ina manufaa makubwa.
Amesema wizara hiyo haina mamlaka ya kupima ardhi,
bali jukumu lipo kwa Wizara ya Ardhi lakini katika uwekezaji wa mipaka wameenda bila kuwa na watalaamu wa wizara hiyo.
Ametoa mfano wa Msitu wa Kazimzumbwi ambao Wizara ya Maliasili ilibadilisha mipaka na kusababisha mgogoro.
Pia, Profesa Tibaijuka ameshauri wizara hiyo kuachana na operesheni kwa sababu ni mambo ya haraka na ya kushtukiza.