Hakika mtoto mdogo halali na pesa, hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya kile kilichowapata Liverpool hii leo. Pamoja na ubora wao wote walikubali kipigo cha mabao 3 kwa 0 kutoka kwa Real Madrid.
Habari kubwa katika mchezo wa leo ilianza dakika ya 26 baada ya Sergio Ramos kumchezea rafu mbaya Mo Salah ambayo ilimfanya kwenda nje dakika 5 baadae, hata hivyo hadi dakika 45 za kwanza zinaisha ilikuwa Real Madrid 0-Liverpool 0.
Dakika ya 51 uzembe wa mlinda lango wa Liverpool Loris Karius ulimfanya Karim Benzema kuwapa Madrid bao la uongozi, bao hili ni la 56 kwa Benzema na anakuwa mchezaji wa pili wa Kifaransa kufunga katika fainali ya CL baada ya Zinedine Zidane.
Dakika ya 55 Sadio Mane aliisawazishia Liverpool na hili likiwa bao lake la 10 katika CL msimu huu na la 20 kwa msimu huu, dakika ya 61 Zinedine Zidane alimnyanyua Gareth Bale aliyekuwa benchi na sub ya Gareth Bale ilibadili kila kitu katika mchezo huu.
Gareth Bale alifunga mabao mawili, na mabao ya Bale yanamfanya kuwa mchezaji wa kwanza kuingia kama sub na kufunga mara mbili na kuufanya mchezo kumalizika kwa Madrid kuibuka kidedea kwa mabao 3-1 huku Zinedine Zidane akiwa kocha wa kwanza kubeba CL mara tatu mfululizo.
Real Madrid wanakuwa timu ya kwanza kubeba kombe la CL mara 3 mfululizo baada ya Bayern Munich 1974-1976, na timu za Uingereza sasa zinakuwa zimepoteza katika fainali 7 za mwisho za Ulaya dhidi ya timu kutoka Hispania.