Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa Mabingwa Ligi Kuu Tanzania Bara Simba SC, Haji Manara amefunguka na kudai angekuwa mtu wa ajabu kama angeondoka wekundu wa Msimbazi bila ya kupata ubingwa wowote wa ligi kuu.
Manara ametoa kauli hiyo muda mchache klabu ya Mabingwa Watetezi Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga kukabidhi rasmi ubingwa kwa watani wao wa Jadi, Simba SC baada ya kuchapwa bao 2-0 na wenyeji wao Tanzania Prisons 'wajela jela' mchezo ulichezwa katika dimba la Sokoine Jijini Mbeya jioni ya Mei 10, 2018.
"Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma, ametusikia na kutupa malipo tuliyokuwa tunastahili, tumepambana lakini niwashukuru sana wachezaji wetu wa Simba kwa kutambua dhamira yetu ya kupata ubingwa. Lakini niwaambie tu kwamba bado hatujaridhika kwasababu tunataka tumalize ligi hii bila ya kufungwa", amesema Manara.
Pamoja na hayo, Manara ameendelea kwa kusema "hakuna mwanasimba yeyote mwenye furaha kama niliyo kuwa nayo mimi maana nimeumia sana ndani ya miaka minne hii, nimetukanwa, nimedhalilishwa na kufedheheshwa sana lakini Mwenyezi Mungu amenilipia. Ningekuwa mtu wa ajabu sana kama ningeondoka Simba bila ya kupata ubingwa wa ligi kuu".
Kwa upande mwingine, Manara amewakataza watu wasimuite msemaji wa mabingwa wa Tanzania bali aitwe msemaji wa mabingwa wa nchi.