Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia amesema ufisadi uliopo katika miradi ya maji nchini unazidi ule wa mchanga wa madini na kushauri Bunge kuunda kamati teule kuchunguza miradi ya maji,
Akichangia bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji mwaka 2018/19, naibu waziri huyo wa zamani wa habari amesema, “miradi mingi ya maji ni zaidi ya makinikia na wakati Bunge linaunda tume hiyo Wizara ya Mambo ya Ndani ijiandae kupanua magereza.”
Akitolea mfano jimboni kwake Nkamia amesema, “pale Goima alipewa ofisa wa Takukuru, halafu sisi tunaonekana kama watu wa hovyo hovyo, waziri (wa Maji, Isaack Kamwelwe) kama utazunguka nchi nzima bila kuunda tume hutoweza, utazunguka, utapanda katika matenki, hutoweza, miradi mikubwa na midogo inapigwa.”
Amesema wananchi hawana uelewa wa utunzaji wa maji, “mnatumia Sh500 milioni kisha mnawakabidhi wanakijiji ambao hawana utaalamu wowote, miezi miwili unaharibika, badilisheni sera, wananchi wanataka maji.”
Mwaka 2017 Rais John Magufuli aliunda kamati mbili kuchunguza biashara ya usafirishaji mchanga wa madini ambao ulizuiwa kusafirishwa nje ya nchi, kamati hizo zilikuja na ripoti ikiwemo iliyobaini kiwango kikubwa na aina nyingi za madini yaliyomo kwenye makinikia.