Nchi ya Burundi leo inapiga kura ya maoni kufanya marekebisho ya katiba ambayo yanaweza kumuweka Rais wa sasa Pierre Nkurunziza madarakani mpaka mwaka 2034
Kwa mujibu wa BBC Kura hiyo itapigwa ya ndiyo au hapana ili kuongeza muda wa Rais kukaa madarakani kutoka miaka mitano mpaka saba katika awamu moja.
Katiba ya sasa imeweka ukomo kwa Rais aliyepo madarakani kuhudumu kwa kipindi cha awamu mbili, kwa mujibu wa mabadiriko yatakayofanywa yatampa uhuru Rais Nkurunziza kugombea tena katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 akiwa kama mgombea mpya na hivyo huenda akatawala mpaka mwaka 2034.
Chama tawala CNDD-FDD kinachoongozwa na Nkurunziza ndicho kinaendesha kampeni ya kuunga mkono upigwaji wa kura ya ndiyo huku kiongozi wa upinzani Agaton Rwasa chini ya mwamvuli wa muunganiko wa vyama vya upinzani ujulikanao kama Amizero y’Abarundi wakihamasisha kura ya hapana.