Wiki moja baada ya Rais John Magufuli kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa thamani ya fedha iliyotumika kujenga ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu cha Elimu cha Mkwawa (Muce), polisi mkoani hapa imemkamata mkandarasi wa ujenzi huo.
Mei 2, akizungumza na wafanyakazi na wanafunzi wa Muce mjini Iringa, Rais Magufuli aliagiza vyombo hivyo ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kufuatilia ujenzi huo uliogharimu Sh8 bilioni.
Sambamba na agizo hilo, pia aliagiza aliyekuwa mkuu wa chuo hicho, Profesa Phillemon Mushi kuhojiwa na mkandarasi kukamatwa.
Akizungumza na wanahabari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire alisema wanamshikilia mkurugenzi mtendaji wa kampuni iliyojenga mradi huo ya MNM Engineering Service, Godwin Mshana (62) akituhumiwa kujenga ukumbi huo chini ya kiwango. Bwire alisema mkandarasi huyo amekamatwa kutokana na agizo la Rais.
“Mei 3 tulimkamata mtuhumiwa na kumuweka chini ya ulinzi,” alisema Kamanda Bwire.
Aliongeza kuwa wameunda kikosi kazi kinachowahusisha wao na Takukuru kwa ajili ya kufanya uchunguzi na utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
Kamanda Bwire alisema msako unaoendelea hivi sasa unawalenga waliohusika na mradi huo wakiwamo waliotoa zabuni.
Akizungumzia suala hilo, Kamanda wa Takukuru mkoani Iringa, Aidan Ndomba alisema, “Kama vyombo vya sheria tumeshirikiana kufanya msako na kuhakikisha tunamkamata mkandarasi baada ya kufuatilia kwa kina juu ya ujenzi huo.”
Alisema Takukuru imefanya kazi kubaini thamani iliyotajwa ambayo alieleza ni kubwa ikilinganishwa na ubora wa jengo.
Ndomba alisema kwa sasa hawawezi kusema ni watu wangapi wanahusika kwa sababu uchunguzi unaendelea.
“Kwa hiyo tutaweza kuona ni uchunguzi unaohusisha watu wengi na fedha nyingi, hivyo baada ya uchunguzi tutaweza kujua ni mtu yupi anahusika na upotevu wa fedha,” alisema.