Rais Magufuli: " Unadaiwa na Jeshi hulipi ??!!, hizo ni dharau...Natoa Mwezi Mmoja"

Rais John Magufuli ametoa  mwezi mmoja kwa taasisi za  Serikali na watu binafsi wanaodaiwa Sh 41.4 billioni na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuhakikisha wanalipa fedha hizo.

Magufuli ametoa maagizo hayo leo Alhamisi Mei 17, 2018 alipokuwa akizindua kituo cha uwekezaji  cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), jijini Dar es Salaam.

Ametoa maagizo hayo baada ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Venance Mabeyo kumuomba kiongozi mkuu huyo wa nchi kusaidia kulipwa kwa madeni hayo.

Awali,  Mabeyo alimueleza Rais kuwa changamoto waliyonayo ni kutolipwa madeni na watu wanaofanya nao kazi.

Amesema kupitia Suma JKT walitengeneza na kukopesha watu mbalimbali na matrekta yenye thamani ya Sh40bilioni na zilizolipwa ni Sh2 bilioni na kubaki deni la Sh 38bilioni.

Ameeleza pia Suma JKT wanaolinda taasisi za Serikali wanadai  Sh 3.4 billion,  hivyo kufanya madeni hayo kwa Sh 41.4 billioni.

 "Tunaomba utusaidie kutia msukumo katika hili kwa sababu taasisi za Serikali zina lugha ya tutalipa tu endeleeni na ulinzi tu" amesema Mabeyo.

Mabeyo amesema kuwa kutokana na hali hiyo wanashindwa kuwalipa pamoja na gharama nyingine za kujikimu.

 "Waziri wa Ulinzi,  Katibu mkuu wa wizara ya Ulinzi waandikieni barua na mnitumie nakala ili niwe nafuatilia watakapokuwa wameanza kulipa.  Nataka fedha hizo zipatikane ili ziweze kutumika kujenga viwanda vingine ."amesema Magufuli akijibu maombi ya Mabeyo.

"Mtu anaanzaje kuacha kulipa fedha ya jeshi,  hii  ni  dharau kubwa,  raia wadharauliwe na Jeshi pia?”

“Niwaombe wote wanaodaiwa madeni kwa kuchukua matrekta, mimi niwape mwezi mmoja. ndani ya mwezi mmoja wawe wamelipa, baada ya mwezi mmoja vyombo vyote vya ulinzi na usalama vianze kuwasaka wote.”

Katika hatua nyingine; Magufuli ameagiza kuwa apelekewe majina ya maofisa waandamizi wa jeshi wastaafu ili awateue kwenye bodi mbali mbali.

"Nileteeni majina yao kwani napata shida kuteua viongozi wa bodi kutokana na tatizo la uadilifu wao. Lakini hawa bado wana uadilifu na nidhamu ya kutosha na bado vijana ambao sidhani kama yupo atakayekataa nikimteua atusaidie,” amesema.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad