Aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe kwa mara ya pili ameshindwa kufika mbele ya Kamati ya Uchunguzi ya Mapato ya Almasi ya Bunge la nchi hiyo.
Mugabe anahitajika kuhojiwa na kamati kuhusu madai ya upotevu wa mapato ya almasi kiasi cha Dola za Kimarekani Bilioni 15 katika kipindi cha utawala wake.
Mugabe alitakiwa kwa mara ya kwanza kutokea mbele ya kamati May 23, 2018 saa 3 asubuhi na kutotokea kwake kulidhaniwa kuwa ni sababu ya uzee hivyo alishindwa kufika muda wa asubuhi.
Kwa mara ya pili Mugabe alitakiwa kufika May 28, 2018 saa 7 mchana lakini pia ameshindwa kufika hivyo kama sheria inavyosema ataitwa mara ya 3 kabla vyombo vya dola havijapewa kazi ya kumfikisha Bungeni kwa nguvu.
Rais huyo aliyeongoza kwa muda mrefu hadi alipotolewa madarakani Novemba mwaka 2017, ametakiwa kufika Bungeni hapo tarehe June 11, 2018 bila kukosa.