Sakata la Ngombe Vibudu Waliokutwa Kwenye Lori Wakipelekwa Sokoni Laibuka Bungeni, Serikali yajibu


NA ISMAEL MOHAMED
Zikiwa zimepita siku chache tangu ilipotokea kizazaa cha ng'ombe waliokufa kutaka kuingizwa sokoni, serikali imewaondoa hofu watanzania kuwa nyama inayopatikana nchini ni bora na yenye usalama wa kutosha na kwa namna yoyote hawawezi kula vibudu.


Kauli hiyo imetolewa leo Mei 16, 2018 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh. Luhanga Mpina Bungeni Jijini Dodoma kwenye kikao cha 30 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu la Mbunge wa Mbinga mjini Sixtus Mapunda aliyetaka kusikia kauli ya serikali kuhusiana na jaribio la kuuza vibudu katika machinjio ya Tegeta Jijini Dar es Salaam Mei 13, 2018.

Wakati anajibu swali hilo Waziri Mpina amesema katika machinjio ya Tegeta walilikamata lori likiwa na ng'ombe 54 kati ya hao 12 walikuwa ni mizoga ambapo mizoga hiyo minne ilikuwa imeshachunwa na miwili ilikuwa tayari imeshakatwa katwa vipande.

"Vyombo vyetu vya usimamizi, Mkurugenzi wa Mifugo, TFDA (Mamlaka ya Chakula na Dawa Nchini) na Halmashauri tunao usimamizi madhubuti kwenye machinjio na mabucha yetu katika kuzingatia usalama wa walaji hivyo basi watanzania wote wasipewe mashaka wala hofu na mtu yoyote kwasababu nyama za Tanzania ni bora kwa namna yoyote hawawezi kula vibudu", amesema Mpina.

Aidha, Waziri Mpina amewashauri watanzania waendelee kula nyama za mifugo yao kwa kuwa vyombo vya dola vipo na vinawahakikishia usalama wa kutosha katika masuala hayo.

"Kwa jaribio hili tu tayari ameshafungiwa machinjio yake kutokana na jambo hilo kuwa limefanywa kinyume na sheria za nchi hivyo Wizara yangu pamoja na Halmashauri ya Kinondoni tulichukua maamuzi ya kuyafungia machinjio ya tegeta kwa muda usiojulikana, kuiteketeza mizoga 12 na kuifukia pamoja kumkamata dereva wa lori hilo pia bado tunamtafuta mmliki wa machinjio hayo kwa kuwa alikimbia baada ya tukio kutokea", amesisitizia Mpina.

Kwa upande mwingine, Mpina amesema mpaka sasa hivi serikali imewaondoa watumishi wote waliokuwa katika kizuizi cha Kibaha na kupeleka wengine baada ya tukio hilo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad