Serikali: Hatuna Mpango Wowote wa Kufanya Marekebisho ya Sheria ya Mtandao

Serikali: Hatuna Mpango Wowote wa Kufanya Marekebisho ya Sheria ya Mtandao
Serikali imesema tangu kuanza kwa matumizi ya sheria ya makosa ya mtandao namba 14 ya mwaka 2015, imesaidia kupunguza makosa ya mtandao na upatikanaji wa haki pale mtu anapotenda kosa tofauti na awali hivyo hawana mpango wowote kwa sasa kufanya marekebisho kwenye sheria hiyo.


Kauli hiyo imetolewa leo na Mei 21, 2018 na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa Bungeni Jijini Dodoma kwenye kikao cha 33 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akijibu la nyongeza la Mbunge wa Ubungo Said Kubenea aliyetaka kujua lini serikali itapeleka bungeni mswada wa marekebisho ya sheria mtandao inayobana uhuru wa mwananchi kupata habari.

"Uwepo wa sheria ya makosa ya mtandao Na. 14 ya mwaka 2015 umesaidia kupungua kwa makosa ya kimtandao, upatikanaji wa haki pale mtu anapotenda kosa kwani kabla ya hapo kulikuwepo na changamoto na uanishaji wa makosa na adhabu hali iliyopelekea haki kutopatikana", amesema Kwandikwa.

Pamoja na hayo, Kwandikwa ameendelea kwa kusema "uwepo wa sheria hiyo umewezesha kuimarika kwa matumizi salama ya mtandao na kuleta maendeleo kwa wananchi. Sheria hii ni muhimu sana kwa nchi yetu na badala ya kuwaathiri watumiaji au wananchi imesaidia kupunguza waharifu wa mtandao.....

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi inaonyesha kupungua kwa makosa hayo kwa asilimia 48.9 kati ya Januari hadi Disemba 2017. Hivyo kwa sasa serikali haina mpango wa kupeleka marekebisho ya sheria hiyo bungeni hadi hapo kutakapokuwa na uhitaji wa kufanya hivyo".

Kwa upande mwingine, Kwandikwa amewataka wananchi kutumia fursa chanya zitokanazo na matumizi sahihi ya mitandao kuliko kutumia mitandao hiyo kuvunja sheria za nchi na maadili pamoja na tamaduni za kitanzania.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad