Serikali Kutafuta Muwekezaji Mwingine Mradi wa Mabasi ya Mwendokasi


Serikali Kutafuta Muwekezaji Mwingine  Mradi wa Mabasi ya Mwendokasi
Serikali imesema ipo katika mchakato wa kutafuta muwekezaji mwingine katika awamu ya pili ya mradi wa mabasi ya mwendokasi ikiwa kama njia ya kujaribu kutatua changamoto za usafiri katika Jiji la Dar es salaam.


Hayo yamesemwa Bungeni leo Mei 10, 2018 na Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa katika kipindi cha maswali na majibu na kusema kuwa serikali ikiongeza muwekezaji mwingine katika mradi huo itasaidia kuleta ushindani wa kibiashara baina ya makampuni hayo na hatimaye wananchi watapata huduma bora ya usafiri.

"Tunaendelea kuondoa changamoto za muendeshaji aliyopo sasa, lakini tumeanza utaratibu wa kupata muendeshaji mwingine ili tupate kampuni nyingine iingize mabasi yake, kuimarisha usafiri wa Jijini Dar es salaam lakini suala la miundombinu tutaimalisha na tunajipanga vizuri ili kuhakikisha huduma hii inaendelea kuwanufaisha watanzania", amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa aliongezea kuwa serikali itachukua hatua kwa muwekezaji wa sasa kama akishindwa kuendesha mradi huo.

"Pale ambapo itabainika muendeshaji wa sasa anamatatizo yaliyokithiri, hatuna shida tutamuondoa kwasababu waendeshaji wapo wengi, wapo watanzania na mataifa ya nje wanaweza kuendesha na kuleta mabasi", amesisitiza Majaliwa.

Kumekuwepo na changamoto mbalimbali katika uendeshaji wa maradi huo ikiwemo mgogogro kati ya UDART na kampuni ya ukatishaji tiketi ya za kielektroniki, ubovu wa miundombinu katika ofisi za kampuni hiyo hasa kipindi cha mvua na changamoto ya uchache wa mabasi kwa abiria wakati wa asubuhi na jioni.

Mradi wa mabasi ya mwendokasi kwasasa unasimamiwa na serikali kupitia shirika la usafiri UDA kwa kushirikiana na kampuni binafsi ya DART na kuunda kufanikiwa kuunda kampuni moja ya UDART.

Tags

Top Post Ad

Below Post Ad