Shahidi wa nne upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili Mmiliki wa Shule ya Lucky Vicent, Innocent Mushi pamoja na Makamu Mkuu wa shule hiyo, Longino Nkana ameeleza kuwa gari lililotumika kusafirisha wanafunzi halikuwa na kibali cha kusafirisha wanafunzi hao.
Shahidi huyo, Allen Mwanri ambaye ni Afisa Mfawidhi wa Mamlaka ya Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) ameieleza mahakama hiyo kwamba gari hilo lilipewa leseni ya kusafirisha abiria kutoka wilayani Arusha kuelekea Mirerani mnamo Mei 16, 2016 na iliisha Mei 15, 2017.
Mbele ya hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Arusha, Desdery Kamugisha, shahidi huyo ameieleza mahakama kwamba kwa mujibu wa kumbukumbu za ofisi gari hiyo yenye nambari T871 BYS aina ya Mitsubishi Rosa inamilikiwa na Swalehe Kiluvia.
Shahidi huyo ameeleza kwamba ofisi yake haijawahi kupokea maombi yoyote ya kubadilisha matumizi ya gari hilo tangu leseni iishe muda wake na uhalali wa leseni iliyotolewa ilikuwa ni kusafirisha abiria kutoka wilayani Arusha kuelekea Mirerani.
Shahidi huyo ameeleza kuwa kanuni hizo zimeyataja magari ya abiria lakini sio magari ya kubeba wanafunzi kwa kuwa kanuni za kubeba wanafunzi zimetajwa katika kanuni za SUMATRA za mwaka 2007.
Hakimu Kamugisha ameahirisha kesi hiyo hadi ambapo shahidi mwingine upande wa mashtaka atafika mahakamani hapo kuwasilisha utetezi wake.
Baadhi ya wazazi wa wanafunzi waliofariki katika ajali hiyo walifurika nje na ndani ya mahakama hiyo kwa mara ya kwanza kusikiliza kesi hiyo ambayo imeibua hisia kwa baadhi ya wakazi wa jiji la Arusha.
Shahidi: Gari ya Lucky Vicent Haikuwa na Kibali cha Kusafirisha Wanafunzi 32
May 09, 2018
Tags