Sugu Ampongeza Mwandosya kwa Kumtembelea Gerezani
0
May 24, 2018
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu (Chadema), ameliambia Bunge kuwa wakati akiwa gerezani, alipokea salamu kutoka kwa viongozi na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) huku akimpongeza Prof. Mark Mwandosya kwa kuwa mwana CCM pekee aliyekwenda kumsalimia gerezani.
Akichangia bungeni jijini Dodoma jana mjadala wa makadirio ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka ujao wa fedha, Sugu aliwapongeza viongozi na wabunge wa CCM kwa kumtumia salamu gerezani huku akidai wengi wao waliogopa kwenda kumjulia hali.
Hata hivyo, Sugu alisema CCM waliwakilishwa vizuri na waziri wa zamani Prof. Mwandosya ambaye ndiye pekee wa chama tawala hicho aliyefika gerezani kumjulia hali.
Mbunge huyo ambaye jana alikuwa wa kwanza kuchangia mjadala huo, pia alitumia fursa hiyo kutoa pole kwa wananchi wa Mbeya ambao alidai waliungana naye kutumikia kifungo hicho.
"Nawashukuru watu wote waliopaza zauti zao kulaani kifungo dhidi yangu," alisema Sugu katika maneno yake ya utangulizi kabla ya kujikita katika hoja iliyokuwa bungeni.
Mbunge huyo mwanzoni mwa mwaka huu alihukumiwa kifungo cha miezi mitano gerezani baada ya kukutwa na hatia kisha kuachiwa wiki mbili zilizopita kwa msamaha wa Rais.
Katika mchango wake jana, Sugu alisema matukio ya uhalifu na vifungo dhidi ya wanasiasa kama yeye yanayotokea nchini yanawafanya baadhi ya wawekezaji kuogopa kuja kuwekeza nchini.
Alisema pamoja na kwamba Tanzania inaweza kuwa na jitihada za kuwashawishi wawekezaji kutoka nje kuwekeza nchini, mkakati huo huenda usifanikiwe kwa kuwa wawekezaji wanapenda kuwekeza katika nchi zenye usalama kuliko nchi zenye vurugu na mauaji.
Sugu pia alimshauri Rais aanze kusafiri kwenda nje ya nchi akisisitiza kuwa safari za nje zina faida kama ilivyokuwa enzi za uongozi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete aliyekuwa akisafiri mara kwa mara.
“Pamoja na hayo, serikali haiwatendei haki Watanzania wanaoacha kazi nje na kuja kufanya kazi nchini kwa sababu inataka iwalipe mishahara midogo kama ilivyotokea kwa bosi mmoja wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)," Sugu alisema.
Tags