Waziri Mkuu ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutotumia lugha ya kuudhi au kutumia nguvu pindi wanapokusanya kodi kwa wafanyabiashara.
Badala yake amewataka kuwaelimisha wafanyabiashara juu ya umuhimu wa kulipa kodi na kuwaeleza ni kwa kiasi gani kodi hiyo imefikia.
Waziri Mkuu amesema hayo, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Tunduma, Frank Mwakajoka aliyehoji kuhusu kauli ya Serikali juu ya usumbufu unaoletwa na TRA kwa wafanyabiashara wakati wa kukusanya kodi.
“Serikali imeunda chombo cha kusikiliza kero za wananchi ndani ya TRA lakini kama hawatasikilizwa wanauwezo wa kupeleka kero zao Wizara ya Fedha au kwa kiongozi yoyote mkubwa katika eneo lake kama vile Mkuu wa Mkoa au Wilaya,” alisema Waziri Mkuu.
“Wafanyabiashara wote kwanza wawe na amani katika kufanyabiashara zao nchini na wawekezaji wote waendelee kuwekeza na kuongeza mtaji zaidi ili kuekeza zaidi kwa sababu serikali imedhamiria kufungua milango ya uwekezaji nchini. Tunajua kwamba kodi ni wajibu wa kila mmoja kadiri ya shughuli zake zinazomletea mapato ilivyo kwa ukubwa wake. Kwa hiyo tumeielekeza TRA ihakikishe inapokwenda kukusanya kodi haitumii lugha ya kuudhi wala nguvu”, amesema Majaliwa.
Aidha ameitaka Mamlaka hiyo kufanya kazi kwa weledi na kuwa na mazungumzo na wafanyabiara. Pia tathmini ya kodi isiwe kiwango kikubwa kuliko mtaji wa mfanyabiashara.
Hata hivyo amesema hatua zitachukuliwa kwa yeyote ambaye hatatumia utaratibu mzuri wa kukusanya kodi na amewataka wafanyabiashara kufanya biashara kwa amani.