Tume Ya Haki za Binadamu Yataka Serikali Imrejeshe Miguna Miguna

Tume Ya Haki za Binadamu Yataka Serikali Imrejeshe Miguna Miguna
Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu (KNCHR) imeitaka Serikali kununua tiketi ya ndege kwa ajili ya mwanasheria aliyeondolewa nchini kwa nguvu Miguna Miguna, na kumpatia hati ya usafiri ili aweze kurejea nchini wiki ijayo.

Katika barua iliyoandikwa na mwenyekiti wa KNCHR Kagwiria Mbogori kwenda Idara ya Uhamiaji inasema ni jukumu la serikali kuirahisishia tume hiyo kusimamia kurejea nchini kwa mwanasheria huyo machachari.

Mbogori, katika barua yake, amenukuu amri ya mahakama iliyotolewa kwa manufaa ya Dk Miguna kwamba masharti hayo matatu lazima yatekelezwe kabla ya kurejea kwake.

“Miguna ameiarifu tume kwamba anatarajia kurudi Kenya Mei 16, 2018,” alisema Mbogori katika barua yake iliyoandikwa Mei 5.

“Ili kuisaidia tume iweze kutekeleza maagizo ya mahakama, tume inaihimiza ofisi yake kutii maagizo ya mahakama kwa kumpatia Miguna Miguna hati halali ya kusafiria ya Kenya, kumnunulia tiketi Miguna ya kutoka Toronto, Canada, hadi Nairobi.”

Tume hiyo imeipatia Idara ya Uhamiaji hadi Alhamisi ya Mei 10 kujibu barua hiyo ya kurasa mbili.

Hili litakuwa jaribio jingine kwa Miguna kutaka kurejea kwenye nchi aliyozaliwa. Machi 29, aliondolewa kwa nguvu na kuingizwa kwenye ndege iliyokuwa inakwenda Dubai.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad