KAMPUNI ya Mabasi ya Mwendokasi (UDART) imewaomba wananchi kuwa na subira katika kipindi hiki cha msimu wa mvua kutokana na upungufu wa magari yanayofanya shughuli zake katika jiji la Dar es Salaam kwa vile magari 29 yaliayothirika kutokana na mvua yanafanyiwa matengenezo.
Hayo yameelezwa na leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano (UDART) Deus Bugaywa ambaye aliongeza kwamba kampuni yake inafanya jitihada za kutafuta eneo jingine la muda kwa ajili ya karakana ya matengenezo ya magari kwani kwa sasa hawana sehemu maalum ya kutengenezea magari hayo yanapopata hitilafu.
Ameeleza kuwa wakati jitihada za kutafuta eneo jingine zikiendelea wananchi wawe wavumilivu pale panapotokea uhaba wa magari kwa baadhi ya vituo kwani hata wao wanaumia kuona wakitumia fedha nyingi za kuyapeleka magari hayo kweye matengenezo katika sehemu isiyokuwa rasmi.
Aidha ameeleza kuwa mafuriko yalitokea hivi karibuni yalisababisha mkondo wa maji wa mto Msimbazi ubomoe ukuta wa eneo la miundombinu hiyo ya mabasi eneo la Jangwani na kusababisha sehemu hiyo kujaa matope.