Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage ameungana na mamia ya waombolezaji kuaga miili ya watumishi watatu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) katika ukumbi wa Karimjee jijini hapa.
Watumishi hao meneja wa tafiti na miradi, Martin Masalu, kaimu mkurugenzi wa tafiti, Alvin Said Amir na kaimu mkurugenzi wa uhusiano walifariki dunia Mei 21, 2018 kwa ajali wakati wakitokea Dar es Salaam kuelekea Dodoma.
Akizungumza leo Alhamisi Mei 24, 2018 Mwijage amesema Taifa limepoteza nguvukazi, “kubwa walilolifanya vijana hawa ni kuhakikisha Watanzania wanawekeza ili wasiwe watazamaji na kwa kweli vijana hawa wamejituma na ni wachapakazi.”
Huku akiwaomba watumishi wa kituo hicho kuchapa kazi licha ya kuwapoteza wenzao amesema, “msije mkasema hao wameondoka pengo lao haliwezi kuzibika, fanyeni kazi kama wao huu mzigo ni wenu sasa.”
Mwijage ametoa pole kwa wawekezaji nchini kwa kupoteza watu ambao wamawazoea.
Watu wa kada mbalimbali walishiriki kuaga miili ya watumishi hao.