Baadhi ya wabunge wamemshauri Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kuchukua hatua mbalimbali ili kutatua migogoro ya ardhi nchini.
Wabunge hao wameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma walipokuwa wakichangia bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2018/19
Mmoja wa wabunge waliochangia wizara hiyo ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, Anne Kilango (CCM), ambaye amesema mashamba ya mkonge yaliyoko katika Kata za Makanya na Ndungu wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro, hayana faida kwa wananchi wa kata hizo.
“Kutokana na hali hiyo naiomba Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ichukue hatua ili kuwapa ardhi vijana na wananchi wa kata hizo,”.
Wakati huo huo, Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka (CUF) aliitaka wizara hiyo iongeze kasi ya kutatua migogoro kwa kuwa inarudisha nyuma maendeleo ya wananchi.
Kwa upande wake Mbunge wa Tabora Mjini, Emmanuel Mwakasaka (CCM) aliitaka serikali ifanye uhakiki wa viwanja vyote vyenye migogoro ili kujua wamiliki halali wa maeneo hayo.