Shirika la afya ulimwenguni WHO limesema wagonjwa watatu wa Ebola wametoroka katika kituo cha matibabu nchini Demokrasia ya Congo na kisha kupelekwa kanisani na ndugu zao kwa lengo la kuombewa maradhi yao ambapo wawili kati yao tayari wanaripotiwa kufariki.
Hata hivyo mgonjwa mmoja alirejeshwa Mbandaka kwa matibabu.
Wahudumu wa afya nchini DRC wana wasiwasi kwamba huenda ugonjwa huo ukaenea kwa kasi,kufuatia eneo hilo la Mbandaka kuwa na idadi kubwa ya watu wapatao milioni moja.
Shirika la WHO linasema visa 58 vya Ebola vimetokea tangu mei nane mwaka ulipotokea mlipuko wa ugonjwa huo.
Afisa wa shirika la WHO Eugéne Kabambi amesema ndugu wa wagonjwa hao walifika katika kituo cha matibabu chini ya shirika la madaktari wasio na mipaka na wakadai kuwachukua wagonjwa wao kwenye kuombewa kanisa.
Inadaiwa kuwa walichukuliwa kwa pikipiki na ndipo Polisi wakaanza kuwasaka,ambapo mgonjwa mmoja alikutwa nyumbani na kurejeshwa hospitalini Mei 22 na kisha kufariki jioni ya siku hiyo hiyo.
Familia za ndugu waliokumbwa na Ebola kwa sasa wapo katika uangalizi mkali na baadhi yao wamekwisha kuchanjwa.