Wananchi Wamkataa mganga wa zahanati wakimtuhumu kuiba dawa.

Zahanati ya Kijiji cha Izinga, Kata ya Wampembe wilayani Nkasi mkoani Rukwa, imefungwa kwa muda usiojulikana baada ya wakazi wa kijiji hicho kumkataa mganga wa zahanati hiyo wakimtuhumu kuiba dawa.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, George Fataki alisema wananchi hao wamefikia uamuzi huo baada ya kukamata dawa zikiuzwa katika duka la dawa za binadamu kijijini hapo.

Alisema baada ya wananchi hao kumhoji mmiliki wa duka hilo alieleza kuwa dawa hizo aliuziwa na mganga huyo (jina tunalihifadhi).

Fataki alisema baada ya wananchi hao kupata taarifa hizo walimfuata mganga huyo na walipomhoji alikiri kumuuzia dawa mfanyabiashara huyo baada ya kuona zimekaa muda mrefu bila kutumika na muda wake wa kufikia mwisho wa matumizi ukikaribia.

Alisema Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Hashim Mvogogo alifika kijijini hapo kwa ajili ya shughuli za kikazi na kukuta mgogoro huo.

Kwa mujibu wa Fataki, kaimu mganga huyo alizungumza na wananchi ili wamuache mganga huyo aendelee kutoa huduma katika zahanati hiyo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, Misana Kwangula alikiri kuwapo kwa tukio la kufungwa kwa zahanati hiyo na kuongeza kuwa tayari muuguzi huyo alikwisha fikishwa katika mikono ya sheria.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad