MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohammed Mahmuod, amewaonya watu wanaotumia kivuli cha dini kugombanisha jamii.
Akizungumza katika sherehe za kuadhimisha mwaka mmoja wa kampeni ya Mimi na Wewe iliyokwenda sambamba na chakula cha futari kwa watu mbali mbali, alisema hatowapa nafasi wala kuwavumilia wale wote ambao wanaoitumia dini kwa kisingizio cha kuleta mifarakano ndani ya jamii.
Alisema kuwa mkoa huo utaendelea kuwa wa amani na wala hakuna mtu atakayejaribu kuivunja na kwamba wakaazi wake ni waumini wa dini tofauti,Ayoub aliitaka jamii kuendelea kuwa wamoja ili kuharakisha maendeleo katika nchi yao.
“Umoja na mshikamano ndiyo silaha kuu ya kuleta maendeleo na wananchi kuishi katika hali ya amani,”alisema.
Alisema kuwa kampeni ya Mimi na Wewe imefikisha muda wa mwaka mmoja tangu ilipoanzishwa Mei 21 mwaka jana na tayari watu 15,000 wamenufaika nayo.
Aliongeza kuwa kampeni hiyo imekuwa ikiwasadia watu mbalimbali wanaoishi katika mazingira magumu bila ya ubaguzi wowote pamoja na kupambana na matumizi ya dawa za kulevya.
Akizungumza katika sherehe hizo Naibu Waziri wa Wizara ya Nchi, Afisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalumu za SMZ Shamata Khamis, alisema kuwa kampeni hiyo imesaidia kufanikisha ushirikiano kati ya serikali na watu mbali mbali wakiwemo viongozi wa dini kwa kuwakutanisha na kutatua kero zinazowakabili wananchi.
Kupitia kampeni hiyo, mjane Halima Mohammed mwenye watoto watano yatima ambao kwa sasa hawana makaazi atajengewa nyumba baada ya walipokuwa wakiishi kusombwa na mafuriko.