Wanaume Waliokaidi Wito wa Makonda Waanza Kusakwa

Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limeanza kuwasaka wanaume zaidi ya 1,000 waliokaidi wito wa kufika kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, baada ya kudaiwa kutelekeza watoto.

Wanaume hao ni miongoni mwa waliotajwa na wanawake waliofika kwa Makonda kuomba msaada wa kisheria baada ya kudai kutelekezwa na wenzi wao.

Jumla ya wanawake 17,000 walifika katika ofisi hizo kwa ajili ya kuomba msaada wa kisheria, lakini kutokana na wingi huo ni 7,000 waliohudumiwa.

Makonda aliwaita wanawake na wanaume wenye watoto ambao walitelekezwa na wenza waliozaa nao kwa siku 15 katika ofisi zake jijini Dar es Salaam na wanaume 2008 waliridhia kulea watoto wao.

Mkuu wa Mkoa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akitangaza kamati aliyoiunda kuchunguza tatizo la watoto kutelekezwa, iliyohusisha wanasheria, maofisa ustawi wa jamii na wadau wengine, inayoongozwa na Mwanasheria na Wakili wa Kujitegemea, Albert Msando.

Kamati hiyo yenye wajumbe 11 imepewa mwezi mmoja na itawahoji wananchi waliofika katika ofisi hizo kupata msaada wa kisheria ili kujua wanavyohudumia kwenye ngazi ya Ustawi wa Jamii kabla ya kufika hapo, namna kesi za watoto zinavyoendeshwa na kama sheria iliyopo ina upungufu.

Makonda alisema kati ya idadi ya wanaume hao wapo waliokamatwa kutoka ndani na nje ya mkoa wa Dar es Salaam na kwamba kazi hiyo inaendelea.

“Zoezi la kuwakamata wanaume ambao walikaidi agizo la kuitikia wito wangu linaendelea na tayari nimeshakabidhi majina zaidi ya 1,000 kwa Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa na wengine wameshaanza kukamatwa na wapo kutoka mikoa mbalimbali,” alisema Makonda.

Alisema wapo wanaume waliojitokeza kuitikia wito katika siku ambazo walishafunga kutoa huduma ili nao wasikilizwe.

Aidha alisema katika usikilizaji huo jumla ya familia 4,644 ziliruhusiwa kumaliza kesi zao katika ngazi za manispaaa huku watu 10,000 wakikosa huduma kutokana na ofisi yake kuelemewa na idadi ya watu.

“Sikuweza kuhudumia watu wote waliojitokeza kwasababu walikuwa wengi kuliko uwezo wangu, hivyo watu 10,000 hawakupata huduma na ndiyo sababu ya kuunda kamati hii ili kupata ufumbuzi wa kudumu,” alisema Makonda.

Pia alisema alizisaidia kupata mawakili ambao hawatawatoza fedha familia zaidi ya 100 ambazo ziliamua kumaliza matatizo hayo mahakamani.

“Wanawake wanapata shida na watoto hata wakitaka kudai haki zao mahakamani hawawezi kupata kwa sababu mawakili wanataka fedha kwa hiyo wanawake 100 waliamua kwenda mahakamani nimewatafutia mawakili wa kuwatetea bure,” alisema Makonda.

Aidha, alisema kutokana na kuwapo kwa wimbi la wazazi kutelekeza watoto, kuna ongezeko la zaidi ya watoto 5,000 wa mitaani katika Jiji la Dar es Salaam.

Alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo ndiyo sababu amekuwa akitafuta mbinu mbalimbali za kulitatua na si kupunguza tatizo.

“Watu wanasema Makonda anaanzisha mambo na kuyaacha bila kumalizika, mimi nawaeleza kuwa si kweli, suala hili nilianza nalo kwa kuwaondoa watoto wanaoomba omba barabarani na hii ni sehemu ya nne ya mwendelezo wake,” alisema Makonda.

Pia Makonda alisema baada ya kamati hiyo kukamilisha kazi yake, wataiwasilisha ripoti hiyo kwa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto na Wizara ya Katiba na Sheria ili mapendekezo yake yaweze kufanyiwa kazi.

Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Wakili Msando, aliahidi kuwa ataifanya kazi hiyo kwa uaminifu na uadilifu mkubwa kuanzia jana ingawa ni kazi ngumu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad