Watu watatu wanaotuhumiwa kuwa majambazi wamepigwa mawe hadi kufa na wananchi wa Kijiji cha Bubare Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera.
Watuhumiwa hao waliuawa baada ya kuwekewa mtego kutokana na kuwapo taarifa za wao kutaka kuvamia nyumba ya mmoja wa wakazi wa kijiji hicho kwa nia ya kupora fedha za mauzo ya mifugo.
Baadhi ya viongozi wa Serikali ya kijiji waliojaribu kuwazuia wananchi kuwashambulia watuhumiwa hao, walilazimika kutimua mbio kuokoa maisha yao baada ya kugeuziwa kibao na kuanza kushambuliwa.
Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Denis Mwila alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi wanapowakamata watuhumiwa, badala yake wawafikishe kwenye mikono ya vyombo vya dola kwa hatua za kisheria.
Akizungumzia namna njama za watuhumiwa hao zilivyojulikana na kuwanasa, Mkuu huyo wa wilaya alisema uongozi wa kijiji na jeshi la polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu watu kutaka kuvamia nyumba ya mkazi huyo aliyeuza mifugo yake Mei 16. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi alisema uchunguzi kuhusu tukio hilo unaendelea na kuahidi kutoa taarifa baadaye