Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewatoa hofu waumini wa dini ya Kiislamu akiwaeleza kuwa bei ya bidhaa haitapanda katika msimu wa Ramadhani.
Pia amewaagiza wakuu wa mikoa (RC) na wilaya (DC) kuhakikisha wanasimamia bidhaa ili zisipande bei katika kipindi hicho.
Tayari kumekuwa na hofu miongoni mwa wananchi kuhusu upandaji wa bidhaa za vyakula katika msimu wa Ramadhani, hususan vinavyotumiwa mara kwa mara.
Waziri Mkuu aliyasema hayo jana bungeni mjini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kilichoongozwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Kauli ya Waziri Mkuu ilikuja baada ya mbunge wa kuteuliwa (CCM), Abdallah Bulembo kuuliza kuhusu kupanda kwa bei ya bidhaa katika kipindi cha mfungo.
“Kwa kuwa sisi Waislamu mwezi huu tunakaribia kuingia katika Ramadhani, bado kama siku saba hivi lakini sukari imepanda imefika Sh2,800 hadi Sh3,000, Serikali ina mpango gani katika hili,” alihoji.
Akijibu swali hilo, Majaliwa alisema, “Niwaondolee shaka Watanzania na katika kipindi chote cha Ramadhani sukari itapatikana na (Serikali) itafuatilia mwenendo wa bei ili watu wasipandishe wakijua kuna mfungo kwani watakuwa wanawaadhibu Waislamu.”
Katika swali la nyongeza la Bulembo alimtaka Waziri Mkuu kuwaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kusimamia hilo.
Akijibu, Waziri Mkuu alisema, “Nawaagiza wakuu wa mikoa, wilaya na maofisa biashara kuhakikisha sukari na bidhaa nyingine zote hazipandi bei kwa sababu ya kutaka kuwakomoa Watanzania, kwani malengo ya Serikali ni mazuri.”
Kadhalika, Majaliwa aliionya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutumia lugha rafiki wanapokwenda kudai kodi kwa wafanyabishara huku akisema suala la kukwama kwa meli zilizobeba mafuta ya kula katika Bandari ya Dar es Salaam linashughulikiwa.
Majaliwa alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ambaye alisema kuna taarifa za kupanda kwa bei ya mafuta kutokana na kuzuiwa kwa meli mbili za mafuta ghafi bandarini.
“Bunge lako lilipitisha sheria ya kutoza mafuta ghafi kwa asilimia 10 na mafuta masafi kwa asilimia 25 ili kulinda viwanda vya nchini. Lakini hivi sasa mafuta ya kula yameanza kupanda wakati kuna meli mbili zimezuiwa bandarini. Ili bei isiendelee kupanda, Serikali ina mpango gani na uagizaji wa mafuta,” aliuliza Lema.
Waziri Mkuu alisema atatoa mrejesho kwa kuwa kuna timu ya ufuatiliaji inayofanya kazi hiyo.
Pia, Majaliwa alisisitiza kuwa Serikali itawachukulia hatua maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) wanaotumia lugha chafu kwa wafanyabiashara.
Waziri Mkuu alisema hayo akijibu swali la Mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka aliyetaka kujua Serikali inatoa kauli gani kuhusu matatizo wanayofanyiwa wafanyabishara na TRA hasa ya unyanyasaji na kuongezewa kodi.
Alisema hatua zilizochukuliwa mkoani Lindi kwa watumishi wa TRA zitachukuliwa pia kwa wengine. “Waziri (wa Fedha) mkutane na TRA kuwakumbusha wajibu wao, ili TRA wawe sehemu nzuri kwani kodi inayotolewa na wafanyabiashara inatusaidia kutekeleza miradi yetu hii,” alisema.