Waziri Mkuu: Nitazindua Kampeni Ya Kupima VVU .....Lengo Ni Kuhamasisha Wanaume Wapime Afya Zao, Wajue Hali Zao


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mwezi ujao, atazindua kampeni maalum ya upimaji wa virusi vya UKIMWI (VVU) ambayo imelenga kuwahamasisha wanaume wapime afya zao na kutambua hali zao.

“Serikali tumeandaa kampeni maalum ya kuhamasisha upimaji wa VVU na kuanza matumizi ya dawa za kufubaza VVU mara moja (Test and Treat), hasa kwa wanaume. Kampeni hii itazinduliwa rasmi na mimi mwenyewe jijini Dodoma tarehe 19 Juni 2018,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Mei 30, 2018) wakati akizindua maadhimisho ya miaka 15 tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Kudhibiti Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (PEPFAR) kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.

“Takwimu zinaonyesha watu ambao wako tayari kupima kwa hiyari yao siku zote ni wanawake. Akinababa wakiambiwa hutoa sababu mara hiki, mara kile. Nitoe wito kwa wanaume wote, tubadilike! Ni vema tushiriki kampeni ya wanaume kujitambua na kupima ili tujue hali zetu,” amesema.

Amewataka wadau wote wanaohusika na masuala ya UKIMWI washiriki kikamilifu katika kampeni hiyo baada ya uzinduzi, na pia akawataka Wakuu wa Mikoa mikoa yote nchini wasimamie kampeni hizo muhimu katika mikoa yao hadi ngazi ya vijiji.

Waziri Mkuu amesema ujio wa PEPFAR umeleta mafanikio makubwa katika vita dhidi ya UKIMWI na kupitia shughuli zake, elimu ya kinga na ufahamu kuhusu UKIMWI ilitolewa kwa watu wa rika na makundi mbalimbali ya jamii.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema Tanzania bado inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo ukubwa wa viwango vya maambukizi na kuongezeka kwa idadi ya watu wanaoambukizwa VVU katika baadhi ya mikoa nchini.

Amesema kuna mikoa 14 ambayo kiwango cha maambukizi kiko juu ya wastani wa kitaifa wa asilimia 4.7 na akaitaja mikoa hiyo kuwa ni Njombe wenye asilimia 11.4, Iringa (asilimia 11.3), Mbeya (asilimia 9.3), Mwanza (asilimia 7.2), Kagera (asilimia 6.5) na Katavi (asilimia 5.9). Mikoa mingine ni Shinyanga (asilimia 5.9), Songwe (asilimia 5.8) Ruvuma (asilimia 5.6) Pwani (asilimia 5.5) Tabora (asilimia 5.1) pamoja na Tanga, Dodoma na Geita ambayo yote ina asilimia 5.0 ya maambukizi.

Waziri Mkuu ameitaja mikoa mingine sita ambayo ina ongezeko kubwa la watu wanaoishi na VVU kuwa ni Iringa (asilimia 11.3), Mwanza (asilimia 7.2), Kagera (asilimia 6.5), Tanga (asilimia 5.0), Dodoma (asilimia 5.0) na Manyara (asilimia 2.3).

Amesema takwimu hizo zinaonesha kuwa nguvu na jitihada zaidi zinahitajika katika kuzuia maambukizi mapya ya VVU kwa kuweka utaratibu thabiti na endelevu wa kutoa elimu na hamasa ya kutumia huduma zilizopo za kupambana na UKIMWI nchini. “Kwa hiyo, programu za kinga zinapaswa kuwa endelevu kwenye mikoa yote nchini, hususan mikoa yenye kiwango cha juu cha maambukizi. Pia huduma za ARVs ziendelee kupewa kipaumbele katika mipango yetu,” amesisitiza.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa hafla hiyo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi. Ummy Mwalimu alisema Tanzania kwa sasa ina watu karibu milioni moja ambao wako kwenye matibabu ya kufubaza VVU.

“Kutokana na mpango wa PEPFAR, Tanzania imekwishapokea sh. trilioni 10 tangu mfuko huu uanzishwe mwaka 2003 na matumizi ya dawa za kufubaza VVU yamesaidia kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na UKIMWI kwa asilimia 70, yaani kutoka vifo 110,000 mwaka 2003 hadi kufikia 33,000 mwaka 2016,” alisema.

Alisema kutokana na matumizi ya dawa hizo, maambukizi mapya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto nayo pia yamepungua kutoka asilimia 12 na kufikia asilimia 4.9 hivi sasa.

Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Marekani, Bi Inmi Patterson alisema kati ya sasa na Septemba 2019, PEPFAR inatarajia kutumia zaidi ya sh. trilioni moja (dola za Marekani milioni 512) katika kuboresha huduma za kuzuia maambukizi ya VVU, upimaji na matibabu hapa nchini.

Alisema wanapoendelea na utekelezaji wa kazi za mfuko huo na maadhimisho ya miaka 15 ya PEPFAR, kampeni yao itaendelea kwa mwaka wote wa 2018 na imelenga kupunguza unyanyapaa na tabia ya kuwatenga watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI.

“Kampeni ya PEPFAR15 inalenga kupunguza unyanyapaa, kuongeza upatikanaji na matumizi ya huduma zitolewazo za kukabiliana na VVU. Kila mtu atakayepimwa na kugundulika kuwa ana maambukizi ya VVU, ataanzishiwa matibabu mara moja. Tutafanya kazi na watu wanaoishi na VVU nchini kote ili kusimulia habari nzuri (positive stories) za watu wanaoishi na VVU ambao waliwahi kuwa dhaifu ama wagonjwa lakini sasa wana nguvu na afya; habari za akinamama wanaoishi na VVU na wanapata matibabu ili kuwalinda watoto wao,” alisema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad