Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe ametoa angalizo kwa Watanzania kuwa mitandao ya kijamii ni tofauti kabisa na vyombo vya habari kwa sababu habari zinazotolewa kwenye mitandao ya kijamii ni maoni ya watu binafsi na hayawasilishwi kitaalamu kama vyombo vya habari vinavyofanya.
Waziri Mwakyembe amesema hayo leo Mei 3, 2018 kwenye mdahalo maalumu ulioandaliwa na Shirika la Habari la DW jijini Dar es salaam katika kuadhimisha siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.
Mwakyembe aliulizwa swali kwenye mdahalo huo lililohoji “Je, mitandao ya kijamii ni vyombo vya habari?
“Kwa upande wangu mimi hapana. sio vyombo vya habari, vyombo vya habari vikipata taarifa kutoka kwenye mitandao ya kijamii vinaweka taarifa hiyo kwenye flow (mtiririko) hali ya kuweza kusomwa na wengine ikiwa imezingatia haki ya watu wengine na iwe katika misingi ya uandishi wa habari,“amesema Mwakyembe na kutoa angalizo.
“Mimi najua social media (mitando ya kijamii) ni vitu vingine..Social media sio vyombo vya habari bali ni mkusanyiko watu wenye kutoa duku duku au maoni yao yaani wanakuwa na freedom (uhuru) lakini ukianza kuweka wahariri hiyo sasa inakuwa sio social media tena.“amesema Mwakyembe na kufunga mjadala.