Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Kangi Lugora amesisitiza kwamba serikali iko tayari kuwafunga jela wabunge watakaokwamisha mradi wa Stiggler’s Gorge.
Akijibu hoja za wabunge zilizoelekezwa katika wizara yake katika bajeti ya Wizara ya Nishati bungeni jijini Dodoma leo, Kangi amesema pamoja na malalamiko yanayotolewa na baadhi ya wabunge kwamba mradi huo haujafanyiwa tathmini ya mazingira, serikali imeshafanya tathmini hiyo kwa kuwashirikisha wataalamu mbalimbali.
Hata hivyo, majibu hayo ya Kangi yalionekana kuwakera baadhi ya wabunge wa upinzani na kulazimika kupiga kelele za kuzomea.
"Piga ua Serikali itatekeleza mradi huu. Tunajua chura wanapiga kelele, ila kelele za chura hazimzuii ng’ombe kunywa maji,” amesema.
Amesema kazi ya wapinzani kuanzia Januari Mosi hadi Desemba, 2018 ni kuipinga Serikali, “Sisi kama Serikali hatutachoka kutoa elimu na kuelimisha wanaopinga mradi huu.
“Hapa lilipo jengo la Bunge kulikuwa na mazingira kama mengine, lakini tukaharibu mazingira, hawa wabunge wanapokaa (wanapoishi) hata kama ni eneo dogo waliharibu mazingira ili kupata nyumba.”
Mbunge huyo wa Mwibara (CCM) amesema tathimini ya mazingira ambayo imefanywa katika mradi huo taarifa yake ni ya kitaalamu, imesheheni wataalamu wa mazingira, wadudu, ikolojia na maji na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) walitoa ushauri kwa mshauri mwelekezi ambaye ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)
“Masuala haya ni ya kitaalamu, Watanzania wasiwe na hofu. Hawa wanaopinga mradi huu ukiwatazama wanahitaji umeme ufike vijijini mwao, wengine ni wachum lakini wanapinga,” amesema.
“Maana yake ni kwamba mradi huu wanaona Serikali ikiutekeleza tutakuwa na umeme mwingi, tutakuwa na viwanda, sasa Zitto (Kabwe-mbunge wa Kigoma Mjini) wewe ni mchumi uliyebobea hebu isaidie Serikali kuelimisha wenzako, kwa kuwa ni mpinzani watakuelewa.”
Akimalizia kujibu hoja hizo Lugola amesema, “Serikali itaendelea kujenga mradi huu na wale wote wanaopinga na kama wanatumwa tutawachukulia hatua na kuwapekeka jela.”