KIKOSI cha Yanga kimeondoka kwenda nchini Algeria kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wapinzani wao, USM Alger huku wachezaji saba wakidaiwa kugomea safari hiyo.
Yanga ambayo iliondoka jana Alhamisi, inatarajiwa kuvaana na Alger katika mchezo wa Kundi D utakaopigwa keshokutwa Jumapili, wakiwa kundi moja na timu za Rayon Sport ya Rwanda na Gor Mahia ya nchini Kenya.
Wachezaji hao waliobaki jijini Dar ni Kelvin Yondani, Ibrahim Ajibu, Papy Kabamba Tshishimbi, Thabani Kamusoko, Beno Kakolanya, Obrey Chirwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Akizungumza na Championi Ijumaa, kocha mpya wa timu hiyo raia wa DR Congo, Zahera Mwinyi, alisema wachezaji hao wamebaki Dar na sababu kubwa ni madai ya malipo ya mishahara ya miezi mitatu wanayodai.
Zahera alisema aliona dalili za mgomo wa safari hiyo siku mbili zilizopita baada ya wachezaji hao kugomea mazoezi yaliyofanyika kwenye Chuo cha Polisi, Kurasini, Dar wakiwa katika maandalizi ya mchezo huo.
Aliongeza kuwa, licha ya kukosekana kwa wachezaji hao, kocha huyo amewaahidi Wanayanga kwenda kupambana wakiwa na kikosi hicho walichosafiri nacho kwenda Algeria na kupata matokeo mazuri.
“Nilishangaa kumuona kipa (Youth Rostand) klabuni na kuwepo kwenye msafara wa timu yetu unaokwenda Algeria, kwani ni kati ya wachezaji walioshindwa kufanya mazoezi ya mwisho tukijiandaa na mechi hii, hivyo ninajisikia faraja.
“Niseme kuwa, licha ya wachezaji hao kugoma tunakwenda huko kucheza kwa tahadhari kwa maana ya kushambulia kwa tahadhari huku tukijilinda kuhakikisha tunapata matokeo mazuri.
“Kikubwa mashabiki wa Yanga watuombee tunakwenda kupambana, na jambo la kushukuru tunaanzia ugenini katika mashindano hayo, hivyo tutajitahidi tunapambana na kupata matokeo mazuri,” alisema Zahera.
Kikosi kilichosafiri kwenda Algeria ni makipa; Rostand, Ramadhani Kabwili na mabeki wa pembeni ni Hassan Kessy, Juma Abdul, Hajji Mwinyi, Gadier Michael.
Mabeki wa kati; Andrew Vincent ‘Dante’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na viungo ni Said Makapu, Raphael Daudi, Pius Buswita.
Washambuliaji ni Yussuf Mhilu, Juma Mahadhi na Yohana Nkomola na mawinga ni Emmanuel Martin na Geofrey Mwashiuya.