Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo) Zitto Kabwe amesema kitendo cha Waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga kuonekana akigonganisha glasi na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kimemtia aibu.
Amesema kitendo hicho huenda kikaibua tafsiri tofauti kwa Palestina ambao kwa muda mrefu nchi hizo mbili zimekuwa na mvutano.
Akizungumza leo Mei 23, 2018 katika mjadala wa bajeti ya wizara hiyo mwaka 2018/19, Zitto amesema Tanzania
ilijenga heshima ya kupigania haki kwa wanyonge tofauti na sasa.
“Tuliweka Mwenge juu ya Mlima Kilimanjaro ili umulike ndani na hata nje ya nchi na ulete upendo pasipo na upendo, matumaini pasipo matumaini, heshima palipo jaa dharau. Ndiyo mambo yaliyopo katika sera ya mambo ya nje,”amesema.
Amesema kuanzia mwaka 2016 Tanzania imeona aibu kupigia kura katika majukwaa ya kimataifa ya kuwaunga mkono wanyonge.
Amesema Dk Mahiga alikuwa Israel wakati akigonganisha glasi na Netanyahu, jambo alilodai kuwa linawaumiza Wapalestina.
“Nchi inaona aibu kulaani mauaji ya wanyonge walionyanganywa nchi yao. Umeonekana (Mahiga) katika televisheni ya Israel ukizungumza bila kusema lolote kuhusu wanyonge (Palestina),” amesema.