Baada ya kufunga mabao mawili yaliyoisaidia Nigeria kushinda 2-0 dhidi ya Iceland, mshambuliaji wa timu hiyo na klabu ya Leicester City Ahmed Musa, amejiwekea rekodi ya kuwa mfungaji wa mabao mengi (4) kwenye Fainali za Kombe la Dunia katika historia ya Nigeria.
Musa amefunga mabao hayo katika mchezo wa kundi D uliomalizika jioni hii dhidi ya Iceland, ambapo sasa timu yake imefikisha alama 3 na kujiweka kwenye nafasi ya kufuzu 16 bora endapo itaifunga Argentina kwenye mechi ya mwisho katika kundi hilo.
Mbali na kuwa mfungaji wa mabao mengi kwenye Kombe la Dunia katika timu ya Nigeria, lakini Musa pia amekuwa mchezaji wa tatu kutoka Afrika kufunga mabao mengi kwenye Kombe hilo akitanguliwa na Roger Milla wa Cameroon mwenye mabao 5 na Asamoah Gyan wa Ghana mwenye mabao 6.
Nigeria sasa inashika nafasi ya 3 katika Kundi D ikiwa na alama 3 nyuma ya Croatia ambao wana alama 6. Argentina na Iceland zinafuatana zikiwa na alama 1 kila timu. Tayari Croatia imeshafuzu hivyo kinachosubiriwa ni kujua kati ya timu hizo tatu nani ataungana na Croatia.