Msanii wa muziki kutoka Marekani, Akon amezindua sarafu yake ya mtandaoni ( cryptocurrency) aliyoipa jina la ‘AKoin’ ambayo amedai kuwa miaka michache baadae itanusuru uchumi wa Afrika.
Akizungumza kwenye tamasha la ubunifu la Cannes Lions siku ya Jumatano iliyopita Akon amesema kuwa mradi huo wa sarafu unakuja na mpango wa kuanzisha mji maalumu ambao wakazi wake watatumia sarafu hizo.
Kupitia ukurasa rasmi wa sarafu hiyo wa akoin.io umeeleza kuwa mji huo utakuwa nchini Senegal na lengo kubwa na mji huo utabeba maudhui kama ya mji wa kusadikika uliooneshwa kwenye filamu ya Black Panther ‘WAKANDA’ .
Tayari Akon ameshakabidhiwa ekari 2000 na Rais wa Senegal, Macky Sall kwa ajili ya mradi huo wa kujenga mji mpya na eneo hilo lipo nje kidogo ya mji wa Dakar.
Mtandao huo umeeleza kuwa wakazi wa mji huo utakaojengwa na Akon watakuwa na uwezo wa kununua na kuuziana bidhaa kutumia sarafu hiyo ya AKoin kwa njia ya simu ili kulinda usalama wao.
Sarafu ya Akoin inakuwa sarafu ya pili ya kimtandao au kidijitali hii ni baada ya sarafu maarufu mtandaoni ya Bitcoin kuzinduliwa miaka 9 iliyopita.
Sarafu ya AKoin na Bitcoin ni sarafu ambazo matumizi yake hayaingiliani na mfumo wa kibenki kama zilivyo sarafu nyingine duniani.
Tayari sarafu hiyo imeanza kufanya kazi unaweza ukajisajili kupitia tovuti yao rasmi ya akoin.io ili kupata maelezo yote kwa kina.
Mradi huo unakuwa wa pili kwa Akon kuuzindua baada ya mradi wake wa kwanza wa Akon Lighting Africa wenye lengo la kupeleka umeme jua vijijini kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.