Muda mfupi baada ya mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali kutolewa nje ya ukumbi wa Bunge na Spika Job Ndugai, amesema chanzo ni uamuzi wake wa kutaka kueleza ukweli kuhusu suala la ushuru wa Korosho.
Bobali ametimuliwa nje ya ukumbi wa Bunge leo mchana baada ya kuibuka mvutano kati yake na Ndugai.
Bobali amesema alisimama kupingana na maelezo yaliyokuwa yakitolewa na mbunge wa Siha (CCM), Dk Godwin Mollel kwa madai kuwa alikuwa akilipotosha Bunge.
“Nilishindwa kuvumilia ndio maana nilitaka kumpata taarifa Dk Mollel kuhusu ukweli wa masuala ya korosho. Sikupendezwa na maelezo yake wakati wa mjadala wa Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2018,” amesema.
“Hata hivyo nashukuru Mungu kwa kuniepusha kwa sababu sitaki kuwa sehemu ya watu watakaopitisha sheria hii ambayo naona inakwenda kuua zao la Korosho hasa kwa watu wa mikoa ya kusini,”amesema Bobali na kusisitiza kuwa sasa anarejea kwa wananchi wa jimbo lake kuwaeleza kuhusu suala la Korosho.