IDARA ya Wanyamapori wilayani Longido kwa kushirikiana na polisi inamtafuta mkazi wa Arusha, Deogratius Loya, kwa tuhuma za kugonga kwa gari pundamilia wawili hadi kufa.
Tukio hilo lilitokea eneo la Laandara ambalo ni tajiri kwa mapito ya wanyamapori wilayani Longido katika barabara ya Arusha-Namanga juzi, ambapo mtuhumiwa huyo alikimbia na kutelekeza gari alilokuwa akiliendesha.
Gari lenye namba za usajili T353 ABG aina ya Toyota Land Cruiser lililokuwa likitoka Arusha kwenda Namanga na kuendeshwa na Loya liliwagonga wanyama hao majira ya asubuhi.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kaimu Ofisa Wanyamapori wilayani hapa, Peter Kubingwa, alisema mtuhumiwa huyo alikimbia na kuacha gari hilo eneo la ajali la Laandara na kwamba anatafutwa na polisi.
Alisema baada ya kulikagua gari hilo walikuta mikataba ya makubaliano ya ukodishaji ya matumizi ya siku 14 kati ya Loya na mmiliki wa gari, Richard Mollel, mkazi wa Arusha.
Kubingwa alisema mkataba huo ulionyesha makubaliano ya malipo ya Sh. milioni 1.5 kwa siku hizo 14.
Alisema mtuhumiwa huyo ameonyesha taswira mbaya kwa nchi kutokana na kufanya tukio hilo la ajali na kukimbia bila kutoa taarifa kituo chochote cha polisi au kwa ofisa yeyote wa wanyamapori.
"Kama tunavyotambua barabara ya Arusha-Namanga sehemu kubwa ni ushoroba wa wanyamapori, mtu huyu ananipa mashaka ya kumhisi ni jangili, kwa sababu haiwezekani afanye tukio hilo na kisha akimbie na kutekeleza gari hapo hapo," Kubingwa alisema.
Alisema endapo dereva anagonga nyara ya serikali ni lazima atoe taarifa kituo cha polisi kilichopo karibu au ofisi yoyote ya serikali.
Aidha, Kubingwa alitoa wito kwa madereva kufuata alama za barabarani pamoja na kuendesha gari kwa umakini, hususan, katika barabara ya Arusha-Namanga kwani sehemu kubwa imetawaliwa na wanyamapori.
“Madereva wanaopata ajali kwa kugonga nyara za serikali watoe taarifa mapema kwani kuchelewa kutoa taarifa ni kinyume cha sheria, hivyo, ukikimbia utatafutwa na ukipatikana sheria itachukua nafasi yake,” alisema.