Chadema kimetafuta mbinu mpya ya kuisambaza hotuba mbadala ya bajeti ya kambi ya upinzani bungeni kwa mwaka 2018/19.
Chadema wamesema kuanzia sasa bajeti hiyo itapatikana katika tovuti maalumu ya chama hicho.
Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni siku chache tangu bajeti hiyo yenye kurasa 521, kuzuiwa kusomwa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Taarifa ya chama hicho iliyotolewa jana Juni 21 na mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Tumaini Makene inaeleza kuwa kama chama kinapinga na kulaani kwa nguvu zote uamuzi huo wa Bunge kuzuia kusomwa kwa hotuba ya bajeti mbadala, kinyume na Kanuni za Bunge.
“Wananchi wamenyimwa fursa adhimu ya kusikia namna ambavyo Chadema na Ukawa wangefanya ili kuwakwamua katika hali ngumu wanayopitia. Tutasambaza hotuba hiyo na kwa sasa tayari inapatikana katika tovuti ya chama,” alisema Makene.
Alisema Spika Job Ndugai alipaswa kujisikia vibaya kwa sababu kambi rasmi ya upinzani bungeni chini ya uongozi wake, ililazimika kujichangisha na kutumia fedha kutoka mifuko ya wabunge wake kutafuta watu wa kuwafanyia utafiti, uchambuzi na kuandika hotuba, jambo ambalo lilipaswa kuwa sehemu ya wajibu wa Ofisi ya Bunge.
“Tunatoa wito kwa Spika Ndugai atambue unyeti wa mamlaka ya mhimili wa Bunge, majukumu ya wabunge na Bunge lote kwa ujumla na asimamie sheria zote,” alisema.