Baada ya Mfungo Kuisha Waislam Watakiwa Kufanya Jambo Hili

Baada ya Mfungo Kuisha Waislam Watakiwa Kufanya Jambo Hili
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewaasa Waislamu na Watanzania wote kwa ujumla kuendelea kutenda mema baada ya kuwa wamejisahihisha na kutubu makosa yao ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Hayo yamesemwa Ijumaa hii na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye amemuwakilisha Rais Dkt. Magufuli kwenye Baraza la Eid El Fitr lililofanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema Viongozi waendelea kuwasihi Waislam wote na Watanzania kwa ujumla kuendelea kuonyesha upendo, umoja na kuvumiliana hasa baada ya kumalizika kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Amesema huruma, ukarimu na ucha Mungu ulioonyeshwa katika kipindi cha mfungo wa Ramadhani, uendelee na uwe sehemu ya maisha ya kila siku na kamwe usiwe umeisha baada ya mwandamo wa mwezi wa mfungo mosi.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa upendo, umoja, utulivu, mshikamano na subra uliooneshwa kipindi chote cha mfungo wa ramadhani ni vema ukaendelezwa kwa sababu ucha Mungu si katika mwezi huo pekee.

Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli ameniagiza kwa kusema ‘’Waislam ni kielelezo cha taasisi za dini zinazozingatia maadili mema, hivyo wachache wasijipenyeze na kuharibu taswira yao. Ninawahakikishia kuwa Serikali iko tayari kushirikiana taasisi yeyote ya dini ambayo itakuwa tayari kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria na taratibu tulizojiwekea nchini’’

Amesema wakati huu wa kusherehekea kumalizika kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni vema wakakumbuka maneno ya Mtume Muhammad (S.A.W) kwamba ‘’Mwenye kufanya maasi siku ya Eid ni sawa na kumuasi Allah Sub-hanahu Wata’ala siku ya kiyama,’’.

Awali, Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally alitoa wito kwa Masheikh wa Mikoa na Wilaya zote nchini wahakikishe kila wanapofanya mikutano yao mada ya amani na kudumisha uzalendo zisikose kwa kuwa ni vitu muhimu.

Top Post Ad

Below Post Ad