Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka 2018/19 Kusomwa Kesho

Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka 2018/19 Kusomwa Kesho
Bajeti  Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/19 ambayo ni ya tatu kwa Serikali ya Rais John Magufuli, itasomwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kesho Alhamisi.

Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema "Juni 16 Waziri wa Fedha na Mipango atasoma Bajeti Kuu ya serikali. Baada ya hotuba hiyo ya Waziri wa Fedha tumewaandalia futari wageni wote waalikwa. Siku hiyo tutakuwa na wageni wengi wa serikali."

Ndugai alisisitiza kwamba wabunge wote wawepo siku hiyo, wakati bajeti itakaposomwa.

Alisema anajua bado kuna hati hati, kuwa huenda sikukuu ya Idd itakuwa Ijumaa, lakini jambo muhimu wabunge wawepo siku ya Alhamisi kwenye hotuba ya bajeti na kisha kwenye futari pamoja na wageni waalikwa.

Alieleza kuwa baada ya hotuba hiyo, kusomwa bungeni ndipo wabunge wanaweza kwenda kuungana na familia na ndugu zao, kusherehekea sikukuu hiyo kubwa, inayoashiria kumalizika kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Akiwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2018/19 kwa wabunge Machi 13, mwaka huu mjini Dodoma, Dk Mpango alieleza kuwa katika bajeti hiyo Serikali inatarajia kukusanya na kutumia Sh trilioni 32.476, ikiwa ni ongezeko la Sh bilioni 764 ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2017/18.

Mpango alitaja vipaumbele vya bajeti hiyo kuwa ni mradi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Stiegler’s Gorge katika Mto Rufiji kitakachozalisha megawati 2,100, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kilometa 300 na Morogoro hadi Makutupora kilometa 336 na uboreshaji wa Shirika na Ndege Tanzania (TTCL).

Pia, ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga, uzalishaji wa makaa ya mawe na umeme Mchuchuma na Liganga, uendeshaji wa shamba la miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari Mkulazi mkoani Morogoro na uboreshaji wa bandari za Tanga, Dar es Salaam na Mtwara.

Tags

Top Post Ad

Below Post Ad