Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limewatoa hofu waislamu wanaotarajia kwenda kwenye ibada ya hijja, likieleza kuwa limejipanga vyema kuhakikisha upungufu uliojitokeza mwaka jana haujirudii.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa halmashauri kuu Bakwata Taifa Sheikh Khamis Mataka leo, wakati akizungumza na waandishi wa habari, na kubainisha kuwa zaidi ya mahujaji 100 mwaka, 2017 walikwama kwenda kufanya ibada hiyo baada ya taasisi ya Twaiba iliyokusanya fedha zao kwa madai ya kuwawezesha kusafiri, kuingia mitini.
Sheikh Mataka amesema kuwa hataki mambo yaliyojitokeza mwaka jana, yajirudie sasa na kwamba Taasisi nne ambazo ni Tanzania Chartable Oraganization, Haji Khikma, Taquwa Haji Group na Almadina Social Services Trust hazitosafirisha mahujaji kwa kuwa hazijakidhi masharti yaliyowekwa.
“Mpaka sasa mambo yote yanakwenda vizuri, hakuna tishio lolote ambalo tumelibani la mahujaji kutosafiri kwa sababu mambo yote yapo katika mstari kuhakikisha kuwa waislamu wanatekeleza ibada hiyo,”amesema Mataka.
Mataka amesema moja ya hatua walizozichukua ni pamoja na kutoruhusu taasisi zisizokidhi vigezo kuwadanganya tena wananchi.
Mataka ameeleza kuwa taasisi 11 pekee kati ya 15 ndizo zilizokidhi vigezo na msharti yaliyowekwa ikiwemo , Alhusna Haji Trust, Shamsul Maarifa Kheri na Tanzania Muslim Development Asociatiaon, Tanzania Muslim Haji Trust.
Mbali na hayo ameweka wazi kuwa swala ya Idd Elf Fitri kwa mwaka huu kitaifa itafanyika jijini Dar es salaam katika viwanja vya mnazi mmoja pamoja na baraza kuu la Eid.