Barua hii ya Romelu Lukaku ikuamshe kijana uliyekata tamaa, pambana, amini inawezekana


Maisha ni safari ndefu sana na njia ya mafanikio ni nyembamba inayopaswa kupambana, kila utakacho kinawezekana ukiweka nia na juhudi, Romelu Lukaku ameandika maisha yake na milima aliyopitia, na huu ndio ujumbe wake.

 “Bado navuta picha miaka kadhaa nyuma nilipokuwa mdogo na maskini, navuta picha nikimkumbuka mama yangu na alivyokuwa akionekana, nilikuwa na miaka sita tu” anaanza kuandika Lukaku.

“Nilirudi kutoka shule kwa ajili ya chakula cha mchana na mezani kulikuwa na chakula kilekile ambacho tunakula kila siku(hawakuwa na uwezo wa kubadili chakula) ni mikate na maziwa, lakini kwa kuwa nilikuwa mtoto sikuwa nawaza kuhusu hilo”

“Siku moja nilirudi nyumbani nikamkuta mama jikoni na box la maziwa kama kawaida yetu lakini safari hii alikuwa akiyachanganya na kitu, sikuelewa ni nini na baada ya muda alileta chakula mezani kama kawaida lakini alikuwa akitabasamu”

“Yalikuwa ni maji, maziwa yaliisha kwenye box ilibidi achanganye na maji, tulikuwa maskini na siku hiyo hatukuwa na uwezo wa kununua hata box lingine la maziwa, hakukuwa na pesa ndipo mama akafanya hivyo”

“Baba yangu alikuwa akicheza mpira lakini baada ya kuacha kucheza soka na pesa zote ziliondoka, nakumbuka kitu cha kwanza kiliondoka kwetu ni king’amuzi cha Tv na kuanzia hapo sikuwa naangalia mpira”

“Kuna wakati ilifikia wakati narudi nyumbani wakati wa usiku taa zote zilikuwa zimezima, hakukuwa na umeme na hali hii ilikuwa ikidumu hata kwa wiki tatu tulikuwa tunaishi na giza, wakati wa baridi nilihitaji maji ya moto lakini hatukuweza kuchemsha na kuoga nilikuwa natumia kopo”



“Mkate nao ulianza kuwa shida kwa familia yangu hivyo ilimbidi mama yangu kuanza kukopa kwenye maduka ya mikate, na wauza mikate walinijua mimi pamoja na kaka yangu mdogo hivyo walimkopesha mama”

“Maisha yalikuwa yakiendelea lakini kumbukumbu ya mama yangu kuchanganya maziwa na maji iliendelea kunijia kichwani na niliamini yatakwisha na nilijua nini napaswa kufanya ,hakika nilijiapiza kumaliza umasikini wa nyumbani”

“Tulikuwa tukikaa gizani mimi na mama na mdogo wangu tukisali na kuamini yatakwisha, siku moja nilirudi kutoka shule nikamuona mama yangu analia, roho iliniuma sana nikashindwa kujizuia nikamuambia Mama siku moja hali itakuwa sawa nitakuja kuichezea Anderchelt na mambo yatanyooka”

“Nilikuwa mdogo nilipoanza kucheza mpira lakini hasira nilizokuwa nazo katika soka zilikuwa kubwa sana, kila mechi kwangu ilikuwa fainali, nikicheza mtaani, shuleni na hata kwenye game ilikuwa kama fainali nilikuwa na uchungu wa mafanikio”

“Wakati naanza kuichezea Lierse watu walikuwa na mashaka na umri wangu, walikuwa wakiuliza cheti changu cha kuzaliwa, baba yangu hakuwepo kwakuwa hakuwa na uwezo wa kusafiri hadi nilipo ilibidi nipambane mwenyewe nitafute cheti nilete, sikuwa na mtu wa kunipambania na nilikuwa na miaka 11 tu”

“Nilitaka kuwa mchezaji bora wa Ubelgiji, haswa nikiwaza panya waliokuwa nyumbani kwetu, nikiwaza namna ambavyo sikuwa na uwezo wa kuangalia Champions League na nikiwaza watu walivyokuwa wananitazama, nilikuwa na hasira sana”

“Nikiwa na miaka 12 nilifunga mabao 76 katika mechi 34, mechi zenyewe nilikuwa navaa viatu vya baba ambavyo tulilingana, na kama tunalingana viatu haikuwa tabu kwangu kuvitumia”

“Mwaka 2002 katika mchezo kati ya Real Madrid vs Bayern Leverkusen nakumbuka kesho yake shuleni kila mtu alikuwa akiongelea kuhusu goli la Zidane, sikuwa nimeangalia kwa kuwa hatukuwa na Tv mechi ila kuficha aibu nikajifanya nimeliona, ilibidi nisubiri kwa siku saba hadi rafiki yangu alipodownload video ya goli lile kwenye simu ndipo nikaliona, sikuweza kuangalia kombe la dunia lakini miaka 12 baadaye niko kombe la dunia”

“Babu yangu mzaa mama aliyeko Congo alinipigia siku moja na huwa tunaongea sana kuhusu soka, lakini safari hii hali ilikuwa tofauti aliniomba nimlinde mwanaye(mama yangu), nilishangaa kwanini anasema vile lakini nikaitika nikamuambia sawa babu nitamlinda mama, cha ajabu siku 5 baadaye babu alifariki”

“Wakati niko Anderchelt U-19 nilikuwa benchi na siku moja nilimuambia kocha naomba nicheze na nakuahidi nikicheza nitafunga mabao 25 kabla ya December, kocha akaniambia usipofikisha 25 utakaa benchi, na mimi nikamuambia nikifikisha utatupikia keki na utasafisha uwanja wa mazoezi akasema sawa, ilipofika mwezi November tayari nlikuwa na mabao 25”

“Nilisaini mkataba wangu na Anderchelt siku yangu ya kuzaliwa nakumbuka nilikimbilia kununua PS, sisahau siku ya kwanza kwenda uwanja wa Anderchelt nilimuambia mtunza vifaa nataka jezi namba 10, akaniliuliza nini? Nikamjibu bila uoga nataka namba 10 akaniambia munaotokea academy munapewa namba 30 na zaidi”

“Nakumbuka wakati wa mchezo wa fainali kila mchezaji alivaa suti kali, ni mimi tu nilivaa tracksuit, kutoka kwenye basi hadi kabati la vifaa vya michezo ni mbali kwahiyo Camera za Tv zilikuwa zikinionesha na nilipofika tu chumba cha kubadilishia nguo zilianza kumiminika message  kama 25 za marafiki wakiniuliza kwanini niko kwenye Tv, hawakuamini na hawakujua naweza chezea Anderchelt”

“Sikiliza,sikuweza kumuangalia Thiery Henry akinyanyasa mabeki kwakuwa hatukuwa na Tv lakini sasa hivi kila saa niko naye katika timu ya taifa na najifunza kutoka kwake, yale mambo ambayo sikuyaona kwenye Tv kwake, leo ananihadithia mwenyewe hakika ni faraja na natamani babu angekuwepo ayaone haya”

“Nashangaa sana baadhi ya watu wa Ubelgiji kunicheka wakati nikikosa namba Chelsea na nilipoenda West Brom, ila fresh kwa kuwa hawakuwepo wakati tunachanganya maji kwenye chakula chetu na kama hukuwepo wakati nahangaika huwezi kunielewa”

Hii leo Romelu Lukaku alifunga mabao 2 wakati Ubelgiji wakiipiga Panama bao 3-0 na sasa ni Jan Ceulemans(6) pekee ndiye ana mabao mengi kuliko Lukaku katika michuano mikubwa ya dunia (Euro na World Cup) kwa Ubelgiji.
Tags

Top Post Ad

Below Post Ad