Bashe ajitofautisha kwa wabunge wenzake


MBUNGE wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), amewataka wabunge wenzake kuiacha Kampuni ya SICPA ya Uswisi iliyopewa tenda ya kutekeleza mradi wa stempu za kielektroniki, ifanye kazi yake. 

Alitoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma juzi alipokuwa akichangia mapendekezo ya bajeti kuu ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha na Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017. 

Alisema wafanyabiashara wana kawaida ya kutumia mianya ya kukwepa kodi na serikali imekuwa na jitihada za kuziba mianya hiyo kwa kuboresha sheria zake na ndiyo maana Waziri wa Fedha na Mpango, Dk. Philip Mpango amekuja na mfumo huo wa stempu mpya za kielektroniki. 

“Mheshimiwa Spika, moja ya eneo ambalo wafanyabiashara hutumia nafasi ya 'ku-avoid' (kukwepa) kodi ni kwenye VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani). Eneo hili liko 'connected' (linaunganishwa) na 'production' (uzalishaji)," Bashe alisema. 

Alimtaka Waziri Mpango kufanyia kazi mawazo yote yaliyotolewa na wabunge, akisisitiza kuwa tathmini na utendaji kazi unaonyesha maeneo ambayo SICPA imewahi kufanya kazi yamekuwa na mafanikio. 

“Pale ambapo tumejua wamekuwa na kesi na rushwa, Mheshimiwa Spika suala la rushwa ni suala la watu kama mfumo utaruhusu watoe rushwa, waweze 'ku-win' (kushinda) 'more' (zaidi), 'it is our weakness' (ni udhaifu wetu)," Bashe alisema na kufafanua zaidi: 

“Lakini, kama mfumo wao huu utatusaidia kufanya 'production count' (hesabu za uzalishaji), kama utatuongezea mapato, nikuombe Mheshimiwa Waziri, tunapokuja mwaka kesho ambapo tutakuwa na miezi sita ya utekelezaji wa bajeti, tuletee taarifa ya 'performance' (utendaji) wa hii kampuni."

Mbunge huyo alisema ikiwa baada ya miezi sita ya utekelezaji, kampuni hiyo haitafanya vizuri, basi serikali ichukue hatua. 

“Kuhofia kwa sababu watu watatoa rushwa, kama kuna watu walitoa rushwa 'it is their problem' (ni tatizo lao), watu wetu wakipewa rushwa 'it is our problem' (ni tatizo letu), tuwaache wafanye kazi,”alisema Bashe. 

Katika mjadala huo, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi 'Sugu', alidai asilimia 98 ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi wamejawa unafiki kwa kuwa wanapokuwa nje wanalalamika mambo hayaendi vizuri, lakini wakifika ndani ya Bunge wanasifia. 

"Mheshimiwa Spika, asilimia 98 ya wabunge wa CCM wamejaa unafiki, huko nje tukiwa tunakunywa chai kantini, wanalalamika mambo yanavyokwenda lakini wakija humu ndani hawasemi," Sugu alisema. 

"Nimewagundua wala hawampendi Rais John Magufuli kwa sababu mtu unayempenda siku zote unamweleza ukweli." 

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad